SERIKALI YAANZA UTEKELEZAJI WA MRADI WA BILIONI 4 KUBORESHA HUDUMA YA MAJI MBINGA


Baadhi ya Wenyeviti wa mitaa Halamshauri ya Mji Mbinga Mkoani Ruvuma,wakifuatilia zoezi la utiliaji saini mkataba ya ujenzi wa mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji katika kata nane za Wilaya ya Mbinga.
Na Regina Ndumbaro-Mbinga.
Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma imeingia mkataba na kampuni ya Ngongo Engineering Ltd kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji katika kata nane za Wilaya ya Mbinga.
Hafla ya utiaji saini mkataba huo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbinga, Pendo Damas, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbinga (Mbiuwasa), Mhandisi Yonas Ndomba, na Mkuu wa Wilaya hiyo, Kisare Makori.
Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miezi 12 kwa gharama ya shilingi bilioni 4, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kuboresha huduma za maji safi na salama kwa wananchi.
Baadhi ya wakazi wa kata ya Masumuni wameishukuru Serikali kwa kuleta mradi huo mkubwa wa maji, wakisema utamaliza changamoto ya upatikanaji wa maji katika eneo hilo.
Mkazi wa Masumuni, Moses Mdaka Mapunda, amesema tangu Mji wa Mbinga ulipoanzishwa, haujawahi kupata fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maji kama ilivyo sasa.
Amesisitiza kuwa mradi huo utasaidia kupunguza adha ya upatikanaji wa maji kwa wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakipata maji kwa mgao na mara nyingine kulazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji kwa matumizi ya familia zao.
Kwa upande wake, mkazi mwingine wa kata hiyo, John Yapesa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) tawi la Masumuni, ametoa wito kwa mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha kazi inafanyika kwa haraka na kwa ubora wa hali ya juu.
Ameeleza kuwa upatikanaji wa maji ni tatizo kubwa katika kata hiyo, na wanawake pamoja na watoto hutumia muda mwingi kutafuta maji, jambo ambalo linaathiri maendeleo yao.
Yapesa amependekeza mkandarasi kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kuanza kunufaisha wananchi haraka iwezekanavyo.
Mkazi wa mtaa wa Lusaka, Fides Ngonyani, naye amepongeza juhudi za Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha wananchi wa Mbinga wanapata huduma bora za maji.
Ameomba kuhakikisha mtandao wa mabomba unapanuliwa ili wananchi wengi zaidi wafikiwe na huduma hiyo moja kwa moja kwenye makazi yao badala ya kuendelea kutegemea maji ya mgao.
Pia amewataka wananchi kushirikiana na Serikali kwa kulinda miundombinu ya maji na kutunza vyanzo vya maji ili kuhakikisha mradi huo unadumu kwa muda mrefu.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Mbinga, Ali Simba, amesema utekelezaji wa mradi huu ni sehemu ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM na unadhihirisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuboresha maisha ya wananchi.
Ameeleza kuwa mradi huu ni moja ya mikakati ya kumtua mama ndoo kichwani, huku akiwataka wananchi kushirikiana na Serikali katika miradi mingine ya maendeleo ili kuimarisha ustawi wa jamii na kukuza uchumi wa taifa.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/TlQNVFw
No comments