Breaking News

RC CHONGOLO AITAKA EWURA KUTUPIA JICHO SEKTA YA MAJI NA MAFUTA SONGWE



Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Daniel Chongolo, ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), kutia mkazo katika udhibiti wa huduma za maji na petroli katika mkoa huo, ili wananchi wapate huduma bora.
Ameyasema hayo leo, 5.3.2025, wakati alipotembelewa na Meneja wa EWURA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mha. Karim Ally, ili kujadili utekelezaji na maendeleo ya shughuli za udhibiti katika mkoa huo.
Akizungumzia sekta ya Mafuta ya Petroli, Mhe. Chongolo aliitaka EWURA, kuhakikisha vilainishi vya magari vinavyoingia sokoni ni bora kwa matumizi, kwani kumekuwa na malalamiko ya uwepo wa vilainishi feki katika maeneo ya Songwe.
Aidha, katika sekta ya maji, Mhe. Chongolo aliitaka EWURA kuyapitia kwa makini maombi ya kurekebisha bei, ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vwawa ili waipatie bei mpya inayostahili na kuifanya mamlaka hiyo kufanya kazi kwa ufanisi na kujitegemea, kwani pamoja na mambo mengine asilimia 94 ya watumishi wanategemea mapato ya makusanyo ya mamlaka hiyo.
Mha. Karim aliahidi kufanyia kazi changamoto hizo kwa wakati, kwani ni wajibu wa EWURA kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati na kwa gharama sahihi.

No comments