Rais Dkt. Samia kuisuka upya Muhimbili kwa TZS 1.2 Trilioni
Serikali imenunua na kusimika mtambo wa kisasa wa Angio-Suite Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) uliogharimu TZS. 2 Bil. Hivyo kuiwezesha hospitali kutoa matibabu ya ubingwa bobezi ambayo yalikua hayapatikani hapa nchini hivyo kuongeza idadi ya aina za matibabu ya kibobezi katika eneo hilo ambapo takribani wagonjwa 2,300 wamehudumiwa tangu mtambo huo ulipofungwa mwishoni mwaka 2022.
Akiwasilisha taarifa ya mafanikio ya MNH kwa kipindi cha miaka minne chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Dkt. Rachel Mhaville aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo amesema, kupitia mtambo huo kwa mara ya kwanza nchini hospitali imefanikiwa kuanzisha huduma mpya mbalimbali ikiwamo kuweka mirija myembamba (catheters) kwa kutumia matundu madogo, kutoa damu iliyoganda katika mishipa ya damu pamoja na huduma nyinginezo ambazo zinafanyika kwa ustadi wa hali ya juu.
Dkt. Mhaville ameeleza kuwa mbali na mtambo huo, pia Serikali imenunua mashine mpya ya Mammography iliyogharimu TZS. 1.8 Bil. ambayo ina uwezo wa kupima na kutoa picha zinazoweza kugundua uvimbe kwenye matiti ukiwa katika hatua za awali kabisa ambapo wagonjwa 810 wamehudumiwa tangu mashine hiyo iliponunuliwa mwaka 2024.
“Mashine hii ya Mammography ni ya kisasa na pekee kwa Hospitali za Umma, inatumiwa na madaktari wabobezi wa radiolojia ya wanawake na imeleta mapinduzi katika utoaji wa huduma za uchunguzi wa kisasa kwa wenye magonjwa ya saratani ya matiti, amesisitiza Dkt. Mhaville.
Vilevile katika kipindi tajwa, Serikali imeongeza mashine moja yenye nguvu sumaku 1.5T ambayo inaweza kuona uvimbe mdogo kwenye picha za uchunguzi, iliyogharimu TZS. 2.6 Bil. hivyo kuondoa muda wa wagonjwa kusubiri kutoka siku 4 hadi 5 za awali kufanya kipimo hicho na kufanyika siku hiyohiyo aliyoandikiwa mgonjwa. Ongezeko la mashine ya Kidigitali ya X-Ray iliyogharimu kiasi cha TZS. 358 Mil. imefanikisha hospitali kupunguza muda wa kutoa majibu ya radiolojia kutoka ndani ya saa 48 hadi 24 tangu kipimo kilipofanyika.
Amesema kuwa, Serikali imeongeza mashine moja ya CT-Scan (dual) iliyogharimu TZS. 1.8 Bil. yenye uwezo wa vipande 128 hivyo kuongeza idadi ya wagonjwa wanaopimwa kwa siku kutoka 20 hadi zaidi ya 50 na majibu kupatikana kwa haraka, kumwezesha daktari kufanya maamuzi mapema na wagonjwa kupata matibabu stahiki kwa wakati.
“Vilevile hospitali imefanikiwa kununua vifaa vingine ikiwamo mashine za kusadia wagonjwa kupumua 18 zilizogharimu TZS. 932 Mil, mashine za endoskopia zilizogharimu TZS. 215, vifaa vya maabara TZS. 1.8 Bil hatua iliyowezesha uboreshaji mkubwa wa huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ameongeza Dkt. Mhaville.
No comments