Breaking News

VYANDARUA 1,542,836 VYENYE DAWA KUSAMBAZWA KATIKA MKOA WA SHINYANGA

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Jumla ya vyandarua 1,542,836 vyenye dawa vinatarajiwa kusambazwa katika mkoa wa Shinyanga mwezi huu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali na wadau wake kupambana na ugonjwa wa malaria. 

Taarifa hiyo imetolewa leo Januari 6,2025 wakati wa kikao kazi cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga juu ya kampeni ya ugawaji wa vyandarua vyenye dawa Mkoani Shinyanga.

Katika kikao hicho waandishi wa habari wamepitishwa katika mada mbalimbali ikiwemo hali ya malaria nchini Tanzania na mkakati wa kinga dhidi ya malaria, kampeni ya ugawaji wa vyandarua mkoani Shinyanga, mbinu bora za kuwasilisha taarifa za malaria, taarifa muhimu kwa jamii juu ya kampeni ya ugawaji vyandarua na mchango wa vyombo vya habari katika utoaji wa taarifa za kampeni ya ugawaji vyandarua.

Vyandarua hivi vitasambazwa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, huku lengo likiwa ni kupunguza maambukizi ya malaria.

Usambazaji huu utakuwa sehemu ya mpango wa kitaifa wa kupunguza vifo vinavyosababishwa na ugonjwa wa Malari, ambao bado ni changamoto kubwa katika baadhi ya mikoa ya Tanzania.

Vyandarua vyenye dawa vimekuwa moja ya njia bora za kudhibiti maambukizi ya malaria. 

Serikali ya Tanzania inatarajia usambazaji huu utafikia kaya nyingi zaidi na hivyo kuokoa maisha ya wananchi. Usambazaji huu utafanyika kwa ushirikiano wa karibu na Serikali za Mitaa, na kwamba vyandarua vitasambazwa kwa usawa na kwa kasi ili watu wa maeneo ya vijijini wasiachwe nyuma.

Kwa sasa, wananchi wanahimizwa kutumia vyandarua vyenye dawa, na pia kuendelea kuchukua tahadhari nyingine kama vile kupiga dawa za kuua mbu katika makazi yao na kujiepusha na maeneo yenye maambukizi makubwa.




from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/ISML4xw

No comments