VIDEO:Heche anaswa akitoa kauli za kidhalilishaji kwa Rais Dkt.Samia, CHADEMA watakiwa kuwajibika haraka
Katika hali inayozua maswali mengi kuhusu maadili na mtazamo wa viongozi wa Chadema, sauti iliyorekodiwa imemnasa John Heche, mgombea wa nafasi ya makamu mwenyekiti wa chama hicho, akitoa kauli za kidhalilishaji dhidi ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika sauti hiyo, Heche anadai kwamba Rais Samia hatashinda uchaguzi kwa sababu ni mwanamke na anatoka Zanzibar.
Kauli hizi ni dhihirisho la ukosefu wa heshima kwa wanawake na ubaguzi wa kikanda unaoendelea ndani ya chama cha Chadema. Rais Samia amethibitisha uwezo wake kama kiongozi kwa kufanikisha utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa mafanikio makubwa.
Hata hivyo, kauli kama hizi kutoka kwa viongozi wa Chadema zinaonyesha kuwa, badala ya kushindana kwa hoja na sera, wanategemea propaganda za kudharau jinsia na asili ya mtu.
Hii si mara ya kwanza kwa Chadema kuonyesha ukosefu wa mshikamano wa kitaifa. Maneno haya ya Heche yanathibitisha kuwa chama hicho kina viongozi wanaoeneza ubaguzi badala ya kuhubiri umoja na mshikamano wa kitaifa. Je, huu ndio uongozi wanaotaka Watanzania?
Ni wazi kuwa kauli za Heche si tu zinadhalilisha wanawake wa Tanzania, bali pia zinapuuza mchango mkubwa wa Zanzibar kama sehemu ya Muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika dunia ya sasa, ambapo kila mtu anapaswa kuthamini mchango wa jinsia zote na kila kanda, viongozi wa Chadema wanaonekana kushikilia mitazamo ya kizamani na ya kibaguzi.
Watanzania wanapaswa kujiuliza, iwapo mtu kama John Heche anaweza kutoa kauli hizi akiwa bado mgombea wa nafasi ya uongozi wa juu ndani ya Chadema, itakuwaje chama hicho kikipewa dhamana ya kuongoza nchi?.
Tukumbuke kuwa Rais Samia ameonyesha kuwa jinsia si kikwazo kwa mafanikio, na asili yake ya Zanzibar haijazuia juhudi zake za kuimarisha maendeleo ya taifa letu.
Uongozi wa Chadema unapaswa kuwajibika kwa kauli kama hizi. Hatuwezi kumruhusu mtu mwenye mawazo ya kibaguzi na ya kudhalilisha jinsia kupewa nafasi ya kuongoza. Watanzania wanastahili viongozi wenye maono ya kitaifa, si wabaguzi wenye kueneza chuki dhidi ya wanawake na watu wa kanda fulani.
Chanzo: DiraMakini
No comments