Rais Samia kuongoza wakuu wa nchi Afrika mkutano wa Nishati
Mkutano huu unalenga kuharakisha ufikishaji wa umeme kwa
watu milioni 300 barani Afrika ifikapo 2030 kupitia Mpango Mahsusi ujulikanao
kama Mission 300.
NA ABRAHAM NTAMBARA NA TUNU BASHEMELA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu
Hasan anatarajia kuongoza Wakuu wa Nchi za Afrika katika Mkutano wa Nishati
utakaofanyika Januari 27 hadi 28 Mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Hayo yamebainishwa jana na Msemaji Mkuu wa Serikali na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Gerson Msigwa
akifungua warsha ya Wahariri na Waandishi wa Habari kuelekea Mkutano huo,
jijini Dar es Salaam.
Msigwa alisema kuwa nchi zaidi ya 14 zitashiriki huku Marais
zaidi ya 10 wakitarajiwa kuhudhuria Mkutano huo.
"Tanzania inajivunia kuwa mwenyeji wa mkutano huu
mkubwa unaolenga kuharakisha ukuaji wa mageuzi katika nishati barani Afrika.
Tukio hili linatufanya kuwa kitovu cha mjadala wa kimataifa kuhusu nishati ya
umeme endelevu," alisema Msigwa na kuongeza, "Kwa kushirikiana na
wadau wa kimataifa kama Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), na
Umoja wa Afrika, tunalenga kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme bora,
nafuu, na endelevu kufikia waafrika milioni 300 kufikia mwaka 2030,".
Kwamba kupitia nafasi hii, Tanzania inaonyesha dhamira yake
ya kuwa mstari wa mbele katika maendeleo ya nishati ya umeme barani Afrika,
ikiwemo kuimarisha upatikanaji wa umeme vijijini na mijini.
Msigwa alibainisha kuwa umeme ni uti wa mgongo wa maendeleo
ya kiuchumi na kijamii ambapo alieleza, kupitia miradi mikubwa kama Bwawa la
Kufua Umeme la Julius Nyerere, Tanzania imefanikiwa kuongeza uzalishaji wa
umeme ambao mpaka sasa inazalisha megawati 1,410 kutoka katika mashine sita na
matarajio ni mwaka huu mradi kukamilika.
"Kwani, kwa kuimarisha upatikanaji wa umeme,
tunawawezesha wananchi na wajasiriamali kuchangia kikamilifu katika uchumi wa
taifa, hivyo kuongeza pato la Taifa na kuboresha maisha ya kila Mtanzania.
Zaidi sote tunafahamu kuwa na ajenda ya kusambaza umeme bila kuwa na vyanzo vya
kuzalisha umeme vya uhakika ni dhahiri haiwezi kuwa namashiko," aliongeza
Msigwa
Hivyo, alisema Serikali imejidhatiti kuwa na vyanzo vingi
vya kuzalisha umeme vikiwemo vyanzo ya nishati jadidifu ili kuakisi jitihada za
kuwafikishia umeme wananchi wa mijini na vijijini na kwamba katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2024,
Serikali imefanikiwa kufikisha umeme katika vijiji 12,278, sawa na asilimia
99.7 ya vijiji vyote.
Kadhalika, Vitongoji 32,827 vimefikiwa na umeme kati ya
vitongoji 64,359 sawa na asilimia 51 ikiongeza uwezekano wa wananchi kushiriki
kikamilifu katika shughuli za kiuchumi ambapo hatua hizi zimeimarisha sekta za
elimu, afya, biashara, na usafiri, ambapo taasisi za afya na elimu zaidi ya
12,905 zimeunganishwa na umeme, na kusaidia kuinua viwango vya utoaji huduma
kwa wananchi.
Kwamba zaidi ya hayo, uwekezaji katika vyanzo mbadala vya
nishati kama vile umeme jua, jotoardhi, na upepo unatarajiwa kuongeza
uzalishaji wa umeme kwa megawati 1,100.
Alisema juhudi hizi zinalenga kuvutia uwekezaji katika Sekta
ya viwanda, ambapo idadi ya viwanda vya uzalishaji wa vifaa vya nishati kama
nguzo na nyaya imeongezeka kutoka 23 mwaka 2020 hadi kufikia viwanda 78 mwaka
2024.
"Uzalishaji wa ndani wa vifaa hivi si tu unatoa ajira kwa Watanzania bali pia unapunguza gharama za miradi ya usambazaji nishati vijijini na mijini Ndugu Wahariri na Waandishi wa Habari,Serikali yetu, chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa kinara wa nishati safi ya kupikia Barani Afrika, huku akiweka ajenda ya nishati safi ya kupikia kama mojawapo wa kipaumbele cha kitaifa," alieleza Msigwa na kuongeza,
"Kupitia Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi
ya kupikia wa mwaka 2024 - 2034 Mkakati ambao aliuzindua mwaka 2024, tumedhamiria kufikia asilimia 80 ya kaya kuwa
na nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034. Hatua hii ni muhimu si tu kwa
kuboresha afya za wananchi wetu bali pia kwa kulinda mazingira yetu dhidi ya
uharibifu wa misitu unaosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa,".
"Na hii ndiyo dhana ya uchumi wa kidiplomasia kwa
vitendo. Tunajivunia kuwa sehemu ya mjadala wa huu wa kuwafikishia umeme
waafrika milioni 300 kwani hapa ndipo patakaposainiwa andiko hilo na nchi 14
Afrika, huku ukihudhuriwa na Marais zaidi ya 10 wa Afrika," alisema
Msigwa.
Kwa upande wake Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu wa
Wizara ya Nishati ambaye pia ni Mwenyekiti
wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano huo, Mhandisi Innocent Luoga alisema
katika Bara la Afrika takriban watu milioni 685 bado hawajafikishiwa na huduma
ya umeme kati ya watu zaidi ya Bilioni 1
duniani.
Hivyo Benki ya Dunia (WB) na Benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB) hivi karibuni walitangaza ushirikiano wa kihistoria utakaosaidia
kuharakisha ufikishaji wa umeme kwa watu milioni 300 barani Afrika ifikapo 2030
kupitia Mpango Mahsusi ujulikanao kama Mission 300.
"Mpango huo Mahsusi utasainiwa na nchi 14 ambazo ni
Mali, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ivory Coast, Burkina Faso, Chad,
Liberia, Madagascar, Malawi, Mauritania, Msumbiji, Niger, Nigeria na
Zambia," alisema Mhandisi Luoga.
Hata hivyo alisema Tanzania ambayo inatambuliwa duniani kwa
kufanya vizuri katika Sekta ya Nishati itasaini mpango huo mahsusi kwa kuwa ni
Nchi Mwenyeji wa Mkutano huo muhimu kwa Sekta ya Nishati.
Alisema kuwa kabla ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi kufanyika
Januari 28, 2025 utatanguliwa na Mkutano wa Mawaziri wa Nishati na Fedha
utakaofanyika Januari 27 Mwaka huu.
Akieleza sababu za Tanzania kuwa Mwenyeiji wa Mkutano huu,
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano Waizaya ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki Balozi Noel Kaganda alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi za
Afrika zinazofanya vizuri katika Sekta ya Nishati.
Alisema hadi kufikia Disemba 2024, uzalishaji umeme kwa
Tanzania bara ulikuwa umefikia Megawati 3,169.20, upatikanaji wa umeme
umeongezeka kutoka asilimia 14 mwaka 2011 hadi asilimia 78.4 mwaka 2020.
Kwamba kufuatia Mpango wa Usambazaji Umeme vijijini (REA),
takriban vijiji vyote nchini vimefikiwa
Sababu nyingine ni kuwa Rais Dkt. Samia amekuwa kinara wa
kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo amefanya hivyo kwenye majukwaa mbalimbali ya
kimataifa, ikiwemo COP 27, 28 na 29, Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu
Nishati Safi ya Kupikia (May, Paris), Mkutano wa G20 (Nov, Rio de Janeiro).
No comments