Muswada marekebisho ya sheria za kazi wapita kwa kishindo.
NA MWANDISHI WETU
BUNGE limepitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Kazi wa Mwaka 2024 (The Labour Laws (Amendments) Bill, 2024) uliobadilishwa kwa lengo la kustawisha sekta ya kazi nchini.Katika muswada huo, sheria zilizofanyiwa marekebisho ni Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini, Sura ya 366, Sheria ya Taasisi za Kazi, Sura ya 300 na Sheria ya Usimamizi wa Ajira za Wageni, Sura ya 436.
Awali Waziri wa Madini, Anthony Mavunde akiwasilisha jana Muswada wa Marekebisho hayo kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete alisema Muswada huo umegawanyika katika sehemu nne.
Kwamba sehemu ya kwanza inahusu masharti ya utangulizi ambayo yanajumuisha jina la Muswada na namna ambavyo masharti ya Sheria mbalimbali yanapendekezwa kurekebishwa huku sehemu ya Pili ya Muswada ikipendekeza marekebisho ya kwenye Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini, Sura ya 366 ambapo kifungu cha 4 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuboresha na kuongeza tafsiri ya baadhi ya misamiati iliyotumika katika Sheria.
Waziri Mavunde alisema lengo la marekebisho haya ni kutoa ufafanuzi wa matumizi ya misamiati hiyo ambayo imetumika katika Sheria ambapo Kifungu cha 9 kimependekezwa kurekebishwa kwa kuongeza wigo wa tafsiri ya msamiati "senior management employee".
Alisema lengo la marekebisho haya ni kuongeza wigo wa ufafanuzi wa nafasi ya mfanyakazi mwandamizi katika menejimenti kwenye utekelezaji wa haki ya kujiunga katika vyama vya wafanyakazi.
Aliongeza kuwa kifungu cha 14 kinapendekezwa kurekebishwa ili kubainisha aina ya mikataba ya muda maalum ambapo lengo la marekebisho haya ni kuongeza wigo wa mazingira ambayo mtu anaweza kuajiriwa kwa mkataba wa kipindi maalum, ikiwemo mikataba ambayo mwajiriwa anaajiriwa kwa muda ili kuendana na ongezeko la wingi wa kazi, kutoa fursa kwa wahitimu wa vyuo ili kuwajengea uwezo na kufanya kazi nyingine za misimu.
Kwamba Kifungu kipya cha 16A kinapendekezwa kuongezwa ili kubainisha mazingira ambayo mwajiri na mwajiriwa wanaweza kuingia katika makubaliano ya namna watakavyofanya kazi katika hali ya dharura inayoweza kuathiri uzalishaji mahali pa kazi.
Kwamba lengo la marekebisho haya ni kuhakikisha ulinzi wa ajira na usalama wa mfanyakazi mahali pa kazi, kuwezesha uzalishaji na kupunguza athari kwa waajiri wakati wa magonjwa ya milipuko na matukio ya dharura.
Waziri Mavunde alibainisha kuwa Kifungu cha 33 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuongeza muda wa likizo ya uzazi kwa mwajiriwa ambaye atajifungua mtoto njiti kwa kujumuisha katika likizo yake ya uzazi muda uliobaki kufikia wiki arobaini za ujauzito.
Alisema lengo la marekebisho haya ni kulinda ustawi na afya za watoto wanaozaliwa kabla ya wakati ambao wanahitaji muda wa kutosha wa uangalizi wa mama, ambapo awali katika Muswada ilipendekezwa muda wa wiki thelathini na sita za ujauzito kama ukomo wa muda wa mtoto kutimia.
Hata hivyo, baada ya majadiliano na Kamati, Serikali ilikubaliana na mapendekezo ya kuongezwa muda huo hadi kufikia wiki arobaini.
Vilevile, Serikali ilikubaliana na pendekezo la Kamati la kuongeza muda wa likizo ya Baba ambaye atapata mtoto njiti, ambapo, badala ya likizo ya muda wa kawaida wa siku 3 atapata siku saba ambapo mapendekezo haya yamejumuishwa katika Jedwali la Marekebisho la Serikali.
Kwmaba Kifungu kipya cha 34A kinapendekezwa kuongezwa ili kumwezesha mwajiri kumpatia mwajiriwa likizo bila malipo isiyozidi siku thelathini ambapo lengo la marekebisho haya ni kuweka mazingira mazuri yatakayomwezesha mwajiriwa kupata likizo bila malipo kutokana na majanga au dharura zinazoweza kujitokeza.
Alibainisha kuwa, Kifungu cha 37 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuweka masharti yanayozuia mwajiri kutoanzisha au kuendelea na shauri la nidhamu dhidi ya mwajiriwa pale ambapo mgogoro huo upo mbele ya Tume au Mahakama ya Kazi.
Alisema lengo la marekebisho haya ni kuzuia uingiliaji wa mchakato wa ushughulikiaji wa migogoro iliyowasilishwa kwenye Tume au Mahakama ya Kazi na kulinda haki za waajiriwa.Waziri Mavunde aliongeza, Kifungu cha 40 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuainisha fidia kulingana na aina ya mgogoro na kuweka ukomo wa chini na wa juu wa fidia inayotolewa kwa mwajiriwa aliyeachishwa kazi isivyo halali ambapo lengo la marekebisho haya ni kuweka mwongozo wa utoaji fidia na kudhibiti utoaji wa fidia kwa kiwango kisicho na uhalisia pale inapothibitika kuwa mwajiriwa aliachishwa kazi isivyo halali.
Kwamba Kifungu cha 41A kinapendekezwa kuongezwa ili kuweka masharti kuhusu afua kwa uvunjaji wa mkataba wa ajira ya muda maalumu ambapo lengo la marekebisho haya ni kutoa mwongozo wa utoaji wa fidia kwa mwajiriwa pale ambapo mwajiri atakiuka vipengele muhim vya mkataba vinavyoweza kupelekea mwajiriwa kuacha kazi.
Aidha, alisema Kifungu cha 71 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuweka masharti ya utaratibu wa kuanza kutumika kwa mikataba ya hali bora inayoingiwa na wakuu wa taasisi za umma huku lengo la marekebisho haya ni kuwianisha masharti ya Sheria hii na utaratibu uliowekwa kwenye sheria zinazosimamia utumishi wa umma.
Kwamba Kifungu cha 73 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuwezesha vyama vya wafanyakazi kwa pamoja kuingia mikataba ya hali bora na mwajiri au vyama vya waajiri kwa ajili ya kuanzisha majukwaa ya ushiriki wa waajiriwa mahali pa kazi ambapo lengo la marekebisho haya ni kuongeza ushiriki wa waajiriwa katika masuala yanayohusu maslahi yao na kuboresha mahusiano eneo la kazi.
Kadhalika Kifungu cha 86 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuweka takwa la pande zote katika shauri kuwepo wakati wa usuluhishi na kuzuia mwajiri kuwakilishwa na mwakilishi binafsi ambapo lengo la marekebisho haya ni kufanikisha migogoro kumalizika katika hatua ya usuluhishi.Vilevile, kifungu hiki kinapendekezwa kurekebishwa ili kuweka ukomo wa muda wa kuwasilisha mgogoro kwa hatua ya uamuzi baada ya usuluhishi kushindikana. Lengo la marekebisho haya ni kuhakikisha migogoro ya kazi inashughulikiwa kwa wakati.
Vifungu vingine vilivyopendekezwa na kufanyiwa marekebisho ni vifungu vya 87, 88, 94 na 97 huku sehemu ya Tatu ya Muswada ikipendekeza marekebisho katika Sheria ya Taasisi za Kazi, Sura ya 300, ambapo kifungu cha 2 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuboresha tafsiri za baadhi ya misamiati iliyotumika katika Sheria.
Kwamba lengo la marekebisho haya ni kutoa ufafanuzi wa matumizi ya misamiati hiyo ambayo metumika katika Sheria ambapo Kifungu cha 9 kinapendekezwa kurekebishwa ili kubadili utaratibu wa vikao vya Baraza kutoka katika utaratibu wa mwaka wa kalenda na badala yake kutumia utaratibu wa mwaka wa fedha. Lengo la marekebisho haya ni kuhakikisha vikao vya Baraza vinaendana na kalenda ya Serikali.
Waziri Mavunde alisema Kifungu cha 15 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuweka masharti ya kumzuia msuluhishi aliyehusika katika usuluhishi wa mgogoro katika ngazi ya usuluhushi kuamua katika ngazi ya uamuzi ambapo lengo la marekebisho haya ni kuepuka mgongano wa maslahi katika uamuzi na kuhakikisha uzingatiaji wa misingi ya haki asili.
Alisema Kifungu cha 16 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuweka masharti ya utaratibu kwa Mwenyekiti kuongoza vikao vya Tume na kama hatakuwepo, wajumbe waliopo watateua mjumbe mmoja kuongoza kikao ambapo lengo la marekebisho haya ni kuongeza ufanisi wa utendaji wa Tume.
Vifungu vingine vilivyopendekezwa na kufanyiwa marekebisho ni Kifungu, cha 19, 20, 27 huku vifungu vya 43 na 44 vikipendekezwa kurekebishwa ili kuondoa cheo cha Naibu Kamishna wa Kazi na kutambua maafisa elimu kazi waliopo chini ya Kamishna wa Kazi kwa lengo la kuendana na muundo wa taasisi unaotumika kwa sasa.
Vifungu vingine vya 45, 45A, 55, na 56 ambapo sehemu ya Nne ya Muswada inapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Usimamizi wa Ajira za Wageni, Sura ya 436 ambapo Kifungu cha 9 cha Sheria hiyo kinapendekezwa kurekebishwa ili kuweka masharti ya kumtaka Raia wa kigeni mwenye kibali cha kazi daraja A anayekusudia kujihusisha na kampuni nyingine anayomiliki hisa kupata idhini ya Kamishna wa Kazi badala ya kibali kingine cha kazi.
Kwamba lengo la marekebisho haya ni kuondoa usumbufu na kuweka mazingira bora ya uwekezaji kwa mwekezaji ambaye ni Raia wa kigeni ambapo mara baada ya kupata kibali cha kazi kwa kampuni moja hatahitajika kupata kibali kingine kwa kampuni nyingine atakayomiliki hisa na vifungu vingine ni vya 10, 12.
Kwa upande wake Kamati Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, ikiongozwa na Mwenyekiti wake Fatuma Toufiq, imepongeza serikali kwa marekebisho hayo na kukubaliana na maoni ya kamati ili kuleta ustawi wa wafanyakazi nchini.
No comments