Breaking News

MENEJA WA WAKALA WA VIPIMO MKOANI RUVUMA KUTOA ELIMU YA UTUMIAJI VIPIMO MWAKA 2025

 

Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Ruvuma Edward Mkanjabi

Na Regina Ndumbaro Ruvuma 

Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Ruvuma Edward Mkanjabi, ameeleza kuwa katika mwaka 2025, Wakala umejipanga kuhakikisha matumizi sahihi ya vipimo katika biashara na sekta nyingine muhimu. 

Aina za vipimo vinavyosimamiwa na Wakala ni pamoja na mizani ya mazao, mita za maji, na pampu za mafuta. 

Hata hivyo amesema changamoto zimeendelea kujitokeza, ikiwa ni pamoja na matumizi ya vipimo batili na upungufu wa uelewa miongoni mwa wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa vipimo sahihi. 

Mkanjabi amebainisha kuwa baadhi ya wafanyabiashara bado hawajahamasika kutumia vipimo sahihi, jambo linaloathiri haki ya mlaji na ushindani wa haki katika soko. 

Ili kukabiliana na changamoto hizi, Wakala wa Vipimo Mkoa wa Ruvuma umeandaa mikakati kabambe kwa mwaka 2025. Mikakati hiyo inajumuisha kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wananchi kuhusu madhara ya kutumia vipimo batili, kufanya kaguzi za kushtukiza katika maeneo ya biashara, na kuhakikisha vipimo vyote vinavyotumika vinakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa. 

Aidha, Wakala umejipanga  kuhakikisha utekelezaji wa sheria na kanuni za vipimo unafuatwa ipasavyo. 

Wakala wa Vipimo Mkoa wa Ruvuma utaendelea kuboresha huduma zake kwa kutumia teknolojia za kisasa na kuwajengea uwezo watumishi wake .

Meneja Mkanjabi ametoa wito kwa wafanyabiashara wote mkoani Ruvuma kuhakikisha wanatumia vipimo sahihi na kufuata sheria na kanuni zilizowekwa. 

Ameonya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wale watakaobainika kutumia vipimo batili au kukiuka taratibu za vipimo,  ili kulinda haki za walaji na kuhakikisha biashara inafanyika kwa uwazi na uaminifu.



from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/0nrDgko

No comments