Mashauriano ya Kisiasa ya Tatu Kati ya Tanzania na Norway yafana
Majadiliano hayo yalilenga kutathmini hali ya uhusiano wao na kuangazia maeneo mapya ya ushirikiano.
Ujumbe wa Tanzania katika majadiliano hayo umeongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo.
Mashauriano hayo yamefanyika ikiwa ni utekelezaji wa Hati ya Makubaliano (MoU) iliyosainiwa mwaka 2017, ambayo iliweka msingi wa mazungumzo ya kisiasa ya kila mwaka kwa ajili ya kuimarisha uhusiano kati ya pande hizo mbili.
Akizungumza katika mashauriano hayo, Mhe. Chumi alibainisha maeneo muhimu ya ushirikiano kati ya Tanzania na Norway, yakiwemo miradi ya maendeleo, biashara, nishati, afya, elimu, mabadiliko ya tabianchi, na kilimo.
Alisisitiza vipaumbele vya pamoja vya mataifa hayo mawili katika kukabiliana na changamoto za dunia kama mabadiliko ya tabianchi, kukuza haki za binadamu, na kudumisha amani na usalama duniani.
Mhe. Chumi alitoa wito kwa juhudi za pamoja ili kukuza fursa hizo hapo alionesha kuongezeka kwa kiwango cha biashara na uwekezaji kati ya pande mbili na kubainisha kuna bado kuna maeneo ambayo bado hayajatumiwa vizuri katika sekta za miundombinu, nishati, usindikaji wa mazao ya kilimo, na ubadilishanaji wa Teknolojia.
Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Norway, Mhe. Andreas Motzfeldt Kravik, alionyesha kujivunia kwa ushirikiano wa muda mrefu kati ya Norway na Tanzania na kusisitiza utayari wa Norway kuendelea kuimarisha uhusiano huo.
Alihimiza ushirikiano zaidi kati ya sekta za serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kushughulikia changamoto za pamoja kama mabadiliko ya tabianchi, umaskini, na magonjwa ya mlipuko.
Mhe. Kravik pia alisifu uongozi wa Tanzania katika hatua za kimataifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kupongeza Mpango wa Nishati Safi ya kupikia unaoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, alitoa shukrani za Norway kwa ziara ya kitaifa aliyoifanya Rais Samia nchini Norway mwaka jana, ambayo aliielezea kuwa iliimarisha msingi wa ushirikiano wa kudumu.
Mashauriano hayo yalihitimishwa kwa pande zote mbili kuthibitisha dhamira yao ya kuendeleza ushirikiano na kutafuta maeneo mapya ya Ushirikiano ili kupata manufaa ya pamoja.
No comments