Gates Foundation yaipongeza Tanzania uboreshaji Afya ya msingi na kupunguza vifo vya Mama na Watoto
Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepongezwa kutokana na jitihada madhubuti za
kuimarisha afya ya msingi na kupunguza idadi ya vifo vya kina mama wajawazito
na watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Hayo
yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Gates Foundation Barani Afrika, Dkt. Paulin
Basinga alipotembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambapo alipata fursa
ya kuona jinsi inavyotoa mchango wake kwa Serikali kuimarisha upatikanaji
huduma ngazi ya afya ya msingi, hospitali za rufaa za mikoa hadi Kanda na
hatimaye kupunguza rufaa za wagonjwa kufika hospitalini hapo ikiwemo kupunguza
rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi.
Dkt. Basinga
amesema taasisi anayoiongoza imefanya kazi na Serikali ya Tanzania katika
maeneo ya uboreshaji programu za kilimo, masuala ya fedha kwa ujumla wake,
sekta ya afya hususani kufanya tafiti zilizoibua afua mbalimbali za kupunguza
vifo vya kina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Katika hatua
nyingine, Dkt. Basinga ameipongeza MNH ambayo ni hospitali ngazi ya juu ya nne
nchini kutokana na huduma za ubingwa na ubingwa bobezi inazotoa kwa wananchi wa
ndani, mataifa jirani, mazingira bora ya utoaji huduma na utayari wa watoa
huduma kuhudumia wananchi katika hospitali hiyo.
No comments