#KAZIINAONGEA

Jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuuza Utalii nchini zimeendelea kuungwa mkono na wadau mbalimbali hususani wanataaluma wa vyuo vikuu nchini lengo likiwa ni kuhakikisha nchi inaongeza watalii.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dodoma (UDOM) Dkt. Betty Amosi Begashe, katika utafiti wa Shahada yake ya Uzamivu aliangazia "Sifa za kijamii na motisha za kusafiri: Chaguo la mwelekeo wa vivutio kati ya watalii wa kimataifa wa kurudi nchini Tanzania" ili kupata majibu ya changamoto ya watalii wengi kuto kurudi tena nchini kutalii na nini kifanyike kutatua changamoto hiyo. 

Akiwa Jijini Dodoma baada ya kutunukiwa Shahada yake hiyo ya uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma Dkt. Begashe amesema kuwa Tanzania inasifika kwa vivutio vya aina mbalimbali lakini idadi ya watalii wanaorudi bado ni ndogo ikilinganishwa na baadhi ya nchi za Afrika ambazo ni washindani wake.

"Hii inaweza kuibua maswali kuhusu ni akina nani hasa hawa watalii wanaorudiarudia kuja kutalii nchini kwa mujibu wa sifa zao za kijamii, na watalii hawa wanakwenda wapi na kwa nini wanachagua mwelekeo fulani wa kivutio ambacho wengine hawakijui," Amesema Dkt. Begashe

Dkt. Begashe ameongeza kuwa utafiti huo unanuia kubainisha mifumo ya vivutio na kuchunguza jinsi sifa za kijamii na motisha za usafiri zinavyoathiri uchaguzi wa vivutio vilivyotambuliwa. 

"Kwa hivyo wauzaji wanaweza kugawa soko hili na watoa huduma za utalii wanaweza kuunda vifurushi maalum vya watalii ili kuhakikisha watalii wanaridhika hali itakayo wavutia kurudi tena nchini" Ameongeza Dkt. Begashe 

Aidha Dkt. Begashe ameshauri wahusika katika sekta ya Utalii kutumia tafiti hiyo ili isaidie kuiwezesha Sekta ya Utalii iweze kuingiza mapato makubwa zaidi ya sasa kwa maslahi mapana ya Taifa na wananchi wake.

*#KAZIINAONGEA*