TAWA YAANZA UTEKELEZAJI WA MAAGIZO YA SERIKALI MAADHIMISHO YA MIAKA 63 YA UHURU
Na.Joyce Ndunguru, Morogoro
Kuelekea maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika, leo Desemba 7, 2024 Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imefanya usafi wa mazingira katika kituo cha Afya Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa usafi wa kituo hicho cha afya, Afisa Mhifadhi Mkuu ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhifadhi, Utafiti na Ujirani Mwema, Omary Msangi amesema kuwa TAWA imetekeleza maelekezo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia Waziri Mkuu, Mhe. Kasim Majaliwa alipozitaka Taasisi zote za Serikali kushehereka maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru kwa kufanya shughuli za kijamii.
"Sisi kama TAWA katika kuunga mkono maelekezo ya Serikali tumechagua kuja katika kituo cha Afya Kingolwira kwa lengo la kufanya usafi wa mazingira yanayoizunguka kituo hiki"Wananchi Mhifadhi Msangi.
Aidha, Msangi ametoa rai kwa wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhifadhi rasilimali za wanyamapori, misitu na mazingira kwa ujumla.
Naye, Mwakilishi wa Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kingolwira, Dkt. Leonard Wambura ameishukuru TAWA kwa kununua vifaa vya usafi sambamba na kufanya usafi wa mazingira katika kituo chao.
" Ninawashukuru sana TAWA kwa nia yao nzuri ya kuja kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika katika kituo chetu na tunawakaribisha tena wakati mwingine"
Aidha, Dkt. alishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha vituo vya afya, vilevile alitoa rai kwa wananchi wa Morogoro kuja kuendelea kuchangia damu kwa ajili ya kuendelea kuokoa Maisha ya mama na mtoto.
Ikumbukwe hivi karibuni pamoja na maelekezo mengine Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) alielekeza maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania yafanyike Kwa ngazi ya Mikoa na Wilaya zote nchini Kwa kufanya shughuli za kijamii zikiwemo upandaji miti, usafi wa mazingira katika maeneo ya kijamii kama vile hospitali, masoko, kambi za wazee na wenye uhitaji maalumu.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/yRSdEAY
No comments