#KAZIINAONGEA

Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imesema itaendeleza jitihada zake za kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara kwa lengo la kuboresha shughuli za biashara, uwekezaji na kukuza uchumi wa nchi.
 
Pia imeahidi kushirikiana na sekta binafsi ili kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara nchini ikiwa ni pamoja kujenga na kuimarisha miundombinu kwa ajili ya usafiri na usafirishaji.
 
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko Disemba 6, 2024 jijini Dar es salaam wakati akifungua Kongamano la Majadiliano ya Biashara na Uwekezaji kati ya Serikali na Sekta Binafsi Mwaka 2024 na Mkutano Mkuu wa 49 wa Mwaka 2024 wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA).
 
Dkt. Biteko ameeleza umuhimu wa sekta binafsi na kusema kuwa Tanzania na Afrika kwa ujumla inakisiwa kuwa na vijana wengi ambao wanaingia katika soko la ajira wanategemea sekta binafsi na ndio maana Serikali imeendelea kushirikiana na kutatua changamoto za sekta binafsi.
 
“ Hivi karibuni mlitoa malalamiko kadhaa ikiwemo ya kukwamisha shughuli za biashara na Serikali imeyatatua kwa kushirikiana nanyi pamoja na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi,” amesema Dkt. Biteko.
 
Ametaja baadhi ya jitihada zilizofanywa na Serikali za kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini kuwa ni pamoja na kufanyiwa marekebisho ya sheria na kanuni 55 na sheria zingine 16 na kanuni zake zinaendelea kufanyiwa kazi.
 
“ Serikali imeondoa mwingiliano wa majukumu na kuanzisha mamlaka kama ile ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA) ili kurahisisha shughuli zenu. Pia, imepunguza idadi ya muda wa kupata huduma kutoka siku 14 hadi tatu na kutoka siku saba hadi tatu za kusafirisha mizigo kutoka Dar es salaam hadi Tunduma.”
 
Pamoja na hayo Dkt. Biteko amefafanua kuwa Wakala wa Usalama Mahala Pa kazi (OSHA) imepunguza tozo 16 za biashara ambazo kupitia hizo Serikali inapoteza mapato kiasi cha shilingi bilioni 37 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi na jitihada za Rais Samia za kuboresha mazingira ya biashara nchini.

*#KAZIINAONGEA*