#KAZIINAONGEA

Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatekeleza miradi yenye thamani ya Shilingi Trilioni 2.9 sawa na Dola za Marekani Bilioni 1.108 katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia katika uendelezaji na uboreshaji wa Miji ili kuhakikisha kunakuwa na utoaji bora wa huduma kwa wananchi wote.

Miradi hiyo inayosimamiwa na Ofisi ya Rais -TAMISEMI na kutekekezwa na TARURA kupitia kikundi kazi cha uratibu wa miradi “projects coordiination team (PCT) “ ambao ni mradi wa Uboreshaji Jiji la Dar es Salaam awamu ya pili (DMDP2) na uendelezaji wa bonde la Mto Msimbazi Mkoani Dar es Salaam pamoja na mradi wa TACTIC unaotekelezwa kwenye miji 45 nchi nzima.

Lengo la miradi hiyo ni kuboresha na kuendeleza huduma za usafiri na usafirishaji pamoja na huduma mbalimbali za kijamii ambapo Disemba 05, 2024 kumeshuhudiwa utiaji saini wa ujenzi wa kituo cha Mabasi Inala pamoja na soko la Mjini Kati katika Manispaa ya Tabora mkoani Tabora.

Wakati wa utiaji saini wa  mkataba huo, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, Zainab Katimba amesema ni matarajio ya Serikali kuwa miradi hiyo italeta mabadiliko chanya kwa wananchi wa Tabora kwani miradi hiyo inaboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kuongeza thamani ya maeneo husika na hivyo kukuza pato la mwananchi mmoja mmoja na la Mkoa kwa ujumla.

Amehimiza pia utunzaji wa miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuwa na tija kwa wananchi.

“ Viongozi  wa Halmashauri zote zinazotekeleza miradi ya TACTIC ni lazima mhakikishe kuwa miradi hii ya masoko na Vituo vya Mabasi inatunzwa na inapokamilika iwe na uwezo wa kujiendesha na kuzalisha mapato kwa Halmashauri zenu, “ amesisitiza Katimba.

Kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha mabasi Inala kutawezesha kuhudumia mabasi na daladala zaidi ya 70 kwa wakati mmoja, maegesho ya magari binafsi 142 pamoja na kuongeza makusanyo ya Halmashauri; kuwezesha mazingira rafiki ya kufikika sambamba na uboreshaji wa huduma nyingine za kijamii ikiwemo chumba cha kutunzia watoto, mifumo ya maji, ufungaji wa taa pamoja na ujenzi wa ofisi mbalimbali.

*#KAZIINAONGEA*