Home
/
Unlabelled
/
WAZIRI TABIA MWITA AKARIBISHA WASHIRIKI WA KONGAMANO LA KISWAHILI KIMATAIFA KUFANYA UTALII TANZANIA.
WAZIRI TABIA MWITA AKARIBISHA WASHIRIKI WA KONGAMANO LA KISWAHILI KIMATAIFA KUFANYA UTALII TANZANIA.
Na Hamis Dambaya, Havana.
Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni,Sanaa na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mhe. Tabia Mwita Maulid ametoa wito kwa wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani walioshiriki tamasha la Kiswahili la kimataifa nchini Cuba kutembelea Tanzania ili kujionea na kufurahia vivutio mbalimbali vya utalii.
Mhe. Tabia ametoa ukaribisho huo kwa wageni wakati akifunga tamasha la Kiswahili la kimataifa lililokuwa likifanyika katika mji wa Havana nchini Cuba ambapo amesema Tanzania imejaaliwa vivutio vingi ambavyo havipo sehemu yoyote duniani.
Ameongeza kuwa watalii wakifika Tanzania ambapo ndipo Kiswahili kinazungumzwa kwa ufasaha pamoja na kujifunza lugha hiyo, watapata fursa ya kujionea vivutio vya utalii ikiwemo mbuga mbalimbali za wanyama, vivutio vya urithi wa utamaduni na malikale na kuona mazingira adhimu ya kisiwa maarufu cha Zanzibar na fukwe zake.
“Njooni Zanzibar ambapo Kiswahili kinazungumzwa kwa ufasaha na mkitoka hapo mtapata fursa ya kutembelea mbuga zetu zilizopo nchini Tanzania ambazo zimesheheni wanyama mbalimbali bila kusahau mlima Kilimanjaro, Ngorongoro, Serengeti,”alisema waziri Tabia.
Katika kongamano hilo ujumbe wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro uliongozwa na Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayeshughulikia Uhifadhi,Utalii na Maendeleo ya Jamii bi Victoria Shayo ambapo pamoja na mambo mengine alishiriki kutoa elimu ya vivutio vya utalii kwa wageni waliotembelea banda la Ngorongoro.
Afisa Masoko Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro bwana Michael Makombe aliwaeleza wageni waliotembelea banda hilo kwamba Ngorongoro imekuwa ikivutia wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani kutokana na kuwa na vivutio vya kipekee ikiwemo bonde la kreta ambalo limesheni wanyama wengi.
Bwana Makombe pia aliwaelezea wageni huo uwepo wa Makumbusho ya Olduvai Gorge ambapo watalii wengi hufika kwa lengo la kupata historia ya chimbuko la binadamu wa kale duniani lakini pia makumbusho hiyo imekuwa ikitumika katika shughuli za kitaaluma kwa watafiti wa masuala ya mambo ya kale na utamaduni.
Kongamano la Kiswahili la Kimataifa limemalizika jijini Havana nchini Cuba siku ya Jumamosi kwa tukio kubwa la onesho la utamaduni wa mswahili na kuhudhuriwa na wageni kutoka nchi mbalimbali duniani likiambatana na mawasilisho yaliyolenga kuongeza idadi ya wazungumzaji wa lugha hiyo ulimwenguni.
WAZIRI TABIA MWITA AKARIBISHA WASHIRIKI WA KONGAMANO LA KISWAHILI KIMATAIFA KUFANYA UTALII TANZANIA.
Reviewed by Tanzania Yetu
on
November 10, 2024
Rating: 5
No comments