WATUMISHI WA AFYA WATAKIWA KUTOA HUDUMA BORA KWA WANANCHI.
#KAZIINAONGEA
Watumishi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, wametakiwa kutoa huduma bora ya Afya kwa wananchi kutokana na kuwa, asilimia 77 hadi 80 ya wananchi wanatibiwa katika ngazi ya afya ya msingi hivyo jukumu.
Ni wazi kuwa, Rais wa awamu ya sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka mkazo katika Sekta ya Afya nchini, kusimamia kwa umakini suala zima la utoaji huduma za Afya kwa Watanzania na kutambua kuwa, Idara hii ya Serikali nyeti na kubwa na ndiyo yenye jukumu la kuwahudumia wananchi wengi walio katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa.
Akitoa maelekezo wakati wa kikao kazi na Watumishi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI kilicholenga kuhimiza uwajibikaji katika eneo la usimamizi wa utolewaji wa huduma za afya msingi nchini, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Afya) Dkt. Grace Magembe amesema, Watumishi wanapaswa kusimamia kikamilifu suala zima la utoaji huduma ya afya kwa wananchi.
Dkt. Magembe amewaelekeza Watumishi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuhakikisha wanafanya vikao kazi kila baada ya wiki mbili ili kuboresha usimamizi wa utoaji wa huduma ya afya msingi nchini.
Amesema, Idara ya afya inawafikia wananchi wengi na si tu kwenye eneo la tiba bali ni pamoja utoaji wa huduma za chanjo, uzazi wa mpango, lishe na ustawi wa jamii, hivyo huduma nyingi wananchi wanazipata kupitia ngazi ya afya ya msingi na hii ni kwa sababu Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya ndio zipo karibu na wananchi.
Amesema, sehemu kubwa ya wananchi wanategemea huduma katika ngazi ya afya ya msingi hivyo ni muhimu kwa watumishi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa na ubora unaotakiwa, zinakidhi matarajio ya wananchi na zinapatikana muda wote.
Amewataka Watumishi hao kitambua kuwa, wamepewa jukumu la kuhakikisha wanasimamia na kuratibu utekelezaji wa afua zote za sekta ya afya, kutekeleza maagizo na maelekezo ya viongozi, kuwasimamia vema watumishi wa sekta ya afya walio katika ngazi ya afya ya msingi ili watoe huduma bora, ikiwa ni pamoja na kupokea maoni na kero za wananchi dhidi ya huduma zinazotolewa.
Sanjari na hilo, Dkt. Magembe amewataka watumishi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kuwa na mawasiliano ya kila siku na watumishi wa sekta ya afya walio katika ngazi ya msingi ili kutatua changamoto wanazoweza kukabiliana nazo wakati wa kuwahudumia wananchi.
Dkt. Magembe amefanya kikao kazi na watumishi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya utekelezaji wa maazimio ya kikao kazi cha Septemba 17, 2024 kilicholenga kuimarisha usimamizi wa huduma za afya msingi nchini.
#KAZINAONGEA
WATUMISHI WA AFYA WATAKIWA KUTOA HUDUMA BORA KWA WANANCHI.
Reviewed by Tanzania Yetu
on
November 16, 2024
Rating: 5
No comments