Breaking News

SERIKALI YAJA NA MWAROBAINI KUDHIBITI UHALIFU MTANDAONI


*Kikosikazi maalum chaundwa, wadau wa mawasiliano waja na maazimio

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imeunda kikosikazi kitakachokuwa na kazi ya kufanya operesheni maalum ya kudhibiti uhalifu mtandaoni.

Hayo yamebainishwa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati yakiwasilishwa maazimio ya mkutano wa wadau wa mawasiliano kuhusu uhalifu mtandaoni.

Mhandisi Masauni alisema kuwa kikosikazi hicho kinaundwa na makatibu wakuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na wenzao kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na wadau wengine.

"Kikosikazi hiki kitaanza kazi mara moja baada ya mkutano huu, Makatibu Wakuu wa Wizara hizi mbili (Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi) wake washirikiane na Maktibu Wakuu wenzao," alisema Mhandisi Masauni.

Waziri Masauni alitaja baadhi ya aina ya uhalifu mmtandaoni kuwa ni utapeli, udhalilishaji na unyanyasaji wa kingono huku akieleza mikoa kinara kwa vitendo hivyo kuwa ni Rukwa, Mbeya, Morogoro na Dar es Salaam.

Alieleza umuhimu wa kushirikiana kwa pamoja wadau wa mawasiliano katika kudhibiti uhalifu mtandaoni kwa sababu uhalifu wa mtandaoni vita kubwa inayokua kwa kasi kubwa.

Hivyo alibainisha kuwa ni wajibu wa Serikali kungeza nguvu katika kupambana na janga hilo ambapo alieleza kuwa katika kukabiliana nalo Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza kwenye kitengo cha uhalifu mtandaoni (Sibercrime) ikiwemo uwekezaji wa mifumo ya kisasa ya TEHAMA.

Hata hivyo alibainisha kila mtu anapaswa kuchukua hatua za kujielimisha kukabuliana na uhalifu huo kutokana na maendeleo ya kasi ya TEHAMA na ameelekeza kila mtumishi wa Wizara na Taasisi zinazohusika na kukabiliana na vitendo hivyo kutoa elimu kwa wananchi ili wewe na uelewa wa kuweza kujilinda wenyewe.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa alitaja baadhi ya maazimio ya Mkutano huo wa wadau wa mawasiliano kuhusu uhalifu mtandaoni kuwa ni pamoja na kuwataka wananchi kuhakiki namba za simu zilizosainia na NIDA zao ili kubaini kama kuna namba ambazo zimasajiliwa na NIDA zao na zinafanya uhalifu ziripotiwe ili zifutwe.

Mengine ni kuwataka wananchi kupokea maelekezo kutoka kwa makampuni ya simu kupitia namba ya 100 pekee na kwamba waepuke kupokea maelekezo kupitia namba tofauti na hiyo.

Kwamba wananchi wanapokutana na uhalifu mtandaoni waweze kuripoti kwa Jeshi la Polisi ili  hatua ziweze kuchukuliwa na kadhalika wasitoe nywira za namba zao kwa watu wengine.

Kwa upande wa maazimio yanayohusu makampuni ya simu ni kwamba yametakiwa kuendelea kufanya usajili wa namba za simu kwa alama za vidole na kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu matumizi sahihi ya mawasiliano.

Kuhusu maazimio yanayohusu Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Waziri Silaa alisema kuwa BoT inatakiwa kuendelea kusajili mawakala wa huduma za kifedha ikiwa ni pamoja na kuwawekea masharti magumu na wananchi kuendelea kupewa elimu kuhusu huduma za kifedha matandaoni.

Kwa upande wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, alisema itaendelea kusimamia vyema Sera ya TEHAMA na kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kukabiliana na uhalifu huo.

No comments