#KAZIINAONGEA

Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka mikakati ya kudhibiti Mawasiliano ya dharura kwa kuanzia Mifumo ya Kiteknolojia ya Mawasiliano inayorahisisha utoaji wa taarifa kwa Umma, na kwa Wataalamu wa Afya pindi dharura inapotokea.

Mkakati huo wa Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (World Health Organisation-(WHO), unaendelea kuimarisha ushirikiano na mahusiano yenye lengo la kuboresha uratibu wa majanga na dharura za afya ya jamii nchini.

Lengo la ushirikiano huo ni kuongeza ufanisi wa mifumo ya Afya ya kukabiliana na majanga mbalimbali  ikiwemo milipuko ya magonjwa yanayoweza kuathiri afya za wananchi.

Hayo yamebainishwa na Dkt. Ahmed Makuwani kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali, Prof.Tumaini Nagu, Mkoani Dodoma, wakati wa zoezi la kupima utayari wa vituo vya oparesheni za dharura za afya ya jamii Duniani.

Dkt. Mukuwani amesema, Serikali na WHO zinashirikiana kuboresha miundombinu ya afya, kama vile vituo vya dharura, Mifumo ya upatikanaji wa dawa na usafiri wa haraka kwa majeruhi au waathirika na dharura za kiafya.

Kupitia ushirikiano huo, Serikali inajitahidi kuwajengea uwezo Wataalamu wa afya wa ndani ya nchi kwa kuwapatia mafunzo na vifaa vya kisasa vinavyohitajika wakati wa majanga.

Hatua hizi ni muhimu ili wananchi wapate huduma za haraka na bora wakati wa dharura, kwani Serikali imeweka mikakati ya kudhibiti mawasiliano ya dharura kwa kuanzisha Mifumo ya Kiteknolojia ya Mawasiliano inayorahisisha utoaji wa taarifa kwa Umma, na kwa wataalamu wa afya pindi dharura inapotokea.

#KAZIINAONGEA