#KAZIINAONGEA

Katika mwendelezo wa kuwatumikia wananchi, Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imepanga kuongeza vivuko sita vidogo Kigamboni Dar es Salaam vitakavyosaidia kurahisisha usafiri na kuondoa uchelewaji wa watu kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwengine

Vivuko hivyo vinatarajiwa kuanza kazi rasmi Januari 2025 kama alivyoelekeza  Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa.

Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kwa kushirikiana Kampuni ya Azam Marine zinaendelea kuboresha utoaji wa huduma za usafiri wa vivuko katika eneo la Magogoni – Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Bashungwa ameyasema hayo alipokuwa akikagua huduma za usafiri wa vivuko na kusema kuwa  kutokana na changamoto iliyopo sasa, kuanzia leo  (Novemba 20, 2024) Azam Marine kwa kutumia Sea Tax itaongeza muda wa kutoa huduma kulingana na ilivyokuwa awali ili kupunguza msongamano wakati wa asubuhi na jioni. 

“Nimeelekeza  kufika Desemba 31, 2024 majengo ya kisasa ya abiria yawe yamekamilika na tuingie mwaka mpya wa 2025 tukiwa na Sea tax za Azam sita, hilo lina maanisha kuanzia Januari 01, 2025 vivuko vitakuwa vinasubiria abiria badala ya abiria kusubiria vivuko ambapo mwananchi atasubiri kivuko kwa dakika zisizozidi 3”, amesema Bashungwa. 

Uboreshaji wa utoaji wa huduma za usafiri wa vivuko unaenda sambamba na ujenzi wa majengo ya abiria ya kisasa na uboreshaji wa majengo yaliyokuwepo ambapo serikali imeagiza  kazi hiyo ikamilike Desemba 31, 2024.

Aidha, Serikali inaendelea na mazungumzo na kampuni ya Azam Marine kwa ajili ya kuboresha huduma ya usafiri wa vivuko kwa wananchi wa Mafia ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji na kuchochea shughuli ya Utalii na Uchumi kwa wananchi wa mkoa wa Pwani. 

Katika hatua nyingine, Bashungwa amekagua ukarabati mkubwa wa Kivuko cha MV Kigamboni katika karakana ya Songoro Marine ambapo amebainisha kuwa Serikali tayari imemlipa kiasi cha Shilingi Bilioni 5.6 kwa ajili ya ukarabati wa vivuko mbalimbali nchini, hivyo amemtaka Mkandarasi huyo kukamilisha ukarabati kwa kivuko hicho kwa wakati ili kiweze kutoa huduma kwa wananchi wa Kigamboni.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala ameeleza ushirikiano na kampuni ya Azam Marine umeongeza utoaji  huduma ya usafirishaji kwa wananchi wakati ukarabati wa Vivuko vya MV Kigamboni na MV Magogoni ukiendelea na kufafanua kuwa changamoto iliyojitokeza imetokana na Sea Tax moja kupata hitilafu.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni Azam Marine, Abubakar Aziz ameeleza kuwa mpaka sasa ujenzi wa majengo ya abiria kwa upande wa Magogoni umefikia asilimia 70 na upande wa Kigamboni umefikia asilimia 60, majengo hayo yatahusisha ofisi za mawakala wa mauzo ya tiketi kwa njia ya kielektroniki.

#KAZIINAONGEA