#KAZIINAONGEA

Katika kipindi cha miaka mitatu tangu aingie madarakani, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea na mkakati wake kuhakikisha tatizo la uhaba wa maji katika maeneo mbalimbali nchini linatoweka kabisa, kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya Maji ambayo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Mkakati huo wa Serikali ya awamu ya sita, umetekelezwa kupitia Sekta ya Maji ambapo kwa Mkoa wa Tanga, Rais Dkt. Samia amelekeza nguvu zake katika Mradi wa Maji wa Kata ya Mswaha
Darajani (Mswaha Darajani Water Intake), Wilayani Korogwe Mkoani Tanga.

Wakati Mradi huo unaendelea, Waziri wa Maji Jumaa Aweso, ametembelea mradi na kuwataka Wakandarasi wa Mradi huo wa Maji wa Mswaha Darajani, kuwatumia vijana wa eneo hilo kufanyakazi mbalimbali zenye kuhitaji ujuzi wa juu au chini katika ujenzi wa Mradi huo.

Amesema, kuna kazi nyingi katika mradi ambazo vijana wa maeneo hayo wanaweza kuzifanya ili kujipatia kipato, lakini pia amewasihi vijana hao kuwa waaminifu watakapopatiwa nafasi hizo za kazi.

Mradi huo wa Maji Mswaha Darajani, unaoendelea kutekelezwa kwa sasa, umeigharimu Serikali zaidi ya Shilingi Bilioni 170 ambao, unategemewa kusambaza maji katika maeneo ya Pangani, Handeni, Muheza na Korogwe Mkoani Tanga, na hivyo kupewa jina la Mradi wa Miji 28.

Waziri Aweso amewataka Wataalamu wa Sekta ya Maji kuhakikisha Wananchi wa Kata ya Mswaha, Wilayani Korogwe Mkoani humo, wananufaika vya kutosha na Chanzo cha Maji Mswaha Darajani (Mswaha Darajani Water Intake) kilichopo katika Kata yao.

Amesema, watu wa eneo hilo wapatiwe maji ya kutosha kwani Rais. Dkt. Samia anatambua kuwa, Wizara ya Maji inajenga miradi ya kimkakati ambapo anahitaji wananchi wa eneo la mradi husika kunufaika.

Aidha, amewataka wananchi wa Mswaha kuwa walinzi wakuu wa mradi huo katika kuujenga na kuutunza mradi kwa kutochafua mazingira yanayozunguka mradi huo.

*#KAZIINAONGEA*