Mtendaji Mkuu wa BRELA Godfrey Nyaisa 





Habari mbalimbali katika picha kwenye ufunguzi wa programu muhimu ya Mafunzo ya Walimu ya ARIPO-WIPO kwa Kituo cha Haki Miliki cha Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam.

MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. William Anangisye, amesema kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania, usimamizi mzuri wa haki miliki unaweza kuleta mabadiliko ya kiuchumi, kuhamasisha maendeleo ya viwanda vya ndani na kuwezesha uuzaji wa tafiti.

Prof. Anangisye amebainisha hayo leo Novemba 4, 2024 akifungua rasmi programu muhimu ya Mafunzo ya Walimu ya ARIPO-WIPO kwa Kituo cha Haki Miliki cha Afrika Mashariki, ambapo amesema kupitia programu hiyo lengo ni kuwapatia kizazi kipya cha walimu ujuzi unaohitajika kukabiliana na changamoto za haki miliki, hususan katika eneo la Afrika.

"Katika uchumi wetu wa kimataifa unaokua kwa haraka, haki miliki inakuwa msingi wa uvumbuzi na ushindani. Nchi zinazoweza kutumia na kulinda haki miliki vizuri ziko mstari wa mbele katika uvumbuzi wa kimataifa. Kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania, usimamizi mzuri wa haki miliki unaweza kuleta mabadiliko ya kiuchumi, kuhamasisha maendeleo ya viwanda vya ndani na kuwezesha uuzaji wa tafiti," amesema Prof. Anangisye na kuongeza,

"Hata hivyo, safari ya kuelekea mfumo thabiti wa haki miliki ina changamoto nyingi. Nchi nyingi za Afrika, ikiwemo Tanzania, bado zinaboresha mifumo yao ya haki miliki ili kupata manufaa haya. Programu hii ya mafunzo ni muhimu, kwa kuwekeza katika walimu wenye ujuzi, tunaweza kujenga nguvu kazi iliyo na uelewa wa kina itakayosaidia kuendeleza mifumo ya haki miliki kote barani,".

Kwamba moja ya mambo muhimu kuhusu mpango huu ni ushirikiano wa kimataifa ambapo washiriki kutoka nchi mbalimbali za Afrika, Uingereza, Ukraine, WIPO, na ARIPO wameweza kubadilishana uzoefu na mbinu bora katika haki miliki, kukuza moyo ya kujifunza na ushirikiano.

Prof. Anangisye ameeleza kuwa ushirikiano wa kimataifa ni muhimu katika kutatua changamoto za haki miliki duniani kwamba masuala kama vile uvunjaji wa haki miliki mipakani na bidhaa bandia yanahitaji juhudi za pamoja kutoka kwa wadau wote, serikali, mashirika ya kimataifa, sekta binafsi, na taasisi za elimu. 

"Napenda kupongeza ushirikiano ulioanzishwa kati ya WIPO, ARIPO, na Serikali ya Tanzania kupitia BRELA, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na taasisi nyingine. Ushirikiano huu unadhihirisha kuwa haki miliki si suala la kitaifa tu, bali ni juhudi za kimataifa zinazohusiana na biashara, uvumbuzi, na ubunifu," ameongeza Prof. Anangisye na kusema,

"Serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa kuimarisha mfumo wa haki miliki kama kichocheo cha ukuaji wa kiuchumi. Tunafanya kazi kwa bidii katika kukagua mifumo ya kisheria na kitaasisi ya haki miliki ili kuendana na viwango vya kimataifa, kama vile Mkataba wa TRIPS. Lengo letu ni kuunganisha haki miliki katika Ajenda yetu ya Viwanda, tukiamini kuwa mfumo thabiti wa haki miliki ni muhimu kwa kufikia malengo yetu ya kuwa uchumi wa kati wa juu,".

Hata hivyo, amesema kuna kazi nyingi za kufanya kwani uelewa na elimu kuhusu haki miliki bado ni mdogo katika sekta fulani kwamba hiyo ni sababu ya kuendelea kujenga uwezo ili kuhakikisha mifumo ya kisheria na kitaasisi sio tu kuwepo, bali pia inafanya kazi ipasavyo na inapatikana kwa wote.

Kwamba hiyo ndiyo sababu Programu ya Mafunzo ya Walimu iliyoanzisha leo ina umuhimu mkubwa ambapo inawakilisha hatua muhimu katika juhudi za kujenga uwezo wa kibinadamu unaohitajika kuendesha maendeleo ya haki miliki Tanzania na katika eneo lote. 

Prof. Anangisye amebainisha kuwa walimu watakaotokana na mpango huo wataenda kufanya kazi ya kufundisha wengine, kueneza maarifa na ufahamu wa haki miliki katika nchi zao na kwa njia hii, athari ya mpango huu itajitokeza mbali zaidi.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili na Leseni za Biashara (BRELA) Godfrey Nyaisa ametoa shukrani kwa Prof. Anangisye kwamba uwepo wake unasisitiza umuhimu wa mpango huo kwa Tanzania na Afrika. 

Amemshukuru pia kwa kuandaa Mafunzo hayo ya Walimu na kwa kuunga mkono kuanzishwa kwa Kituo cha Haki Miliki cha Afrika Mashariki katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo kituo hiki kitaweka fursa nyingi kwa wanafunzi, wanazuoni, SMEs, wabunifu, na jamii kwa ujumla. 

"Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pia kinatoa programu ya Master ya Haki Miliki (MIP) kwa ushirikiano na ARIPO, BRELA, na WIPO, ambayo inaunda kundi la wataalamu wa haki miliki katika kanda yetu. Ningependa pia kuwashukuru wakurugenzi wenzangu na wawakilishi kutoka COSOTA na COSOZA kwa kuendelea kusaidia mipango ya haki miliki. Ushiriki wenu katika mpango huu kama wanafunzi ni wa kutia moyo," amesema Nyaisa.

Kadhalika amemshukuru Mkurugenzi Mkuu wa WIPO Daren Tang, kwa msaada wake katika kukuza ubunifu na haki miliki nchini Tanzania kwamba kupitia Chuo cha WIPO, uketolewa msaada muhimu katika kujenga uwezo katika sekta mbalimbali.