MNH YAJIDHATITI KUENDELEA KUPUNGUZA VIFO VYA WATOTO WACHANGA WANAOZALIWA KABLA YA MUDA
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi
Wataalam wa afya nchini wamesisitizwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kupigania maisha ya watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya muda ili kupunguza vifo vya watoto hao na kuweza kufikia malengo ya mpango mkakati wa mwaka 2030 wa kuwa na vifo vya watoto wachanga chini ya vifo 12 kwa kila vizazi hai 1000 .
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi wakati akifungua maadhimisho ya kuelekea siku ya mtoto aliyezaliwa kabla ya muda (njiti) yaliyofanyika katika Hopsitali ya Taifa Muhimbili –Mloganzila ambayo yameshirikisha wataalam wa afya wa watoto wachanga kutoka MNH Upanga &Mloganzila.
Prof. Janabi ameeleza kuwa, inakadiriwa kwamba kwa kila watoto 1000, kuna watoto wachanga wapatao 24 wanaofariki ndani ya siku 28 za kwanza na kwamba mikakati ya kupunguza vifo hivi haiwezi kuwa endelevu bila kushirikiana wadau katika sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuboresha ujuzi wa kuhudumia watoto hao.
Amefafanua kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imekuwa ikiratibu progamu mbalimbali ambazo lengo lake ni kupunguza vifo vya watoto wachanga na wale wa chini ya miaka mitano, program hizo ni kama kumsaidia mtoto kupumua baada ya kuzaliwa, kupanua huduma za watoto wachanga kwa kujenga wodi za watoto wachanga (Neonatal Units) katika hospitali za mikoa na wilaya, pamoja na kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ya namna ya kuhudumia watoto wachanga (Essential newborn care).
Kwa upande wake Daktari Bingwa Bobezi wa watoto wachanga MNH Upanga Dkt. Martha Mkony amesema katika Afrika karibu mtoto mmoja kati ya kumi huzaliwa kabla ya wakati ambapo watoto hao ukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na matatizo ya kupumua, maambukizi , matatizo ya chakula na hatari za ukuaji wa muda mrefu.
“Hata hivyo pamoja na kuwepo kwa changmoto hizo lakini bado kuna matumaini kupitia juhudi za Serikali kwani kuna maboresho ya kutia moyo katika utunzaji wa watoto wachanga nchini kwa kuboresha vituo vya afya na hospitali za kuhudumia watoto wachanga na kujengwa pamoja na kusomesha wataalam wa afya’’ameeleza Dkt. Mkony
Aidha maadhimisho hayo yameenda sambamba na uzinduzi wa kitengo cha kuhifadhi na kuratibu maziwa ya mama (Lactational Management Unit) kwa la kuhakikisha watoto hao wanapata maziwa ya mama zao kwa wakati kwakua watoto wanaozaliwa kabla ya muda wanakua na uzito mdogo ambao unasababisha kuhitaji kiasi kidogo cha maziwa, kwahiyo hata kama mama anauwezo wa kutoa maziwa mengi kiasi kinachobaki kinahifadhiwa hivyo ni rahisi mama akiruhuisiwa kurejea nyumbani anakwenda na maziwa yake. Hii inasaidia mpango wa kuhakikisha watoto wachanga wanayonyeshwa miezi sita bila kupewa chochote.
No comments