WAWEKEZAJI WAKARIBISHWA KUJENGA VIWANDA UKANDA MAALUM WA KIUCHUMI KAHAMA
Akizungumza leo, Novemba 20, 2024, katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, wakati wa Mkutano ulioandaliwa na Ubalozi wa Australia nchini Tanzania, ambako katika mkutano huo kati ya Serikali ya Tanzania na Wawekezaji kutoka Australia mijadala mbalimbali iliibuliwa kuhusu fursa zinazopatikana katika Sekta ya Madini hapa nchini.
Dkt. Kiruswa amesema kuwa, eneo hilo lina miundombinu tayari, ikiwemo barabara, umeme hali inayotoa nafasi bora ya kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani na miradi mingine ya uwekezaji ambapo tayari baadhi ya Kampuni ikiwemo Kampuni ya Tembo Nickel Refining Limited zimeshaanza utaratibu wa kujenga kiwanda cha kusafisha makinikia kutoka Mgodi wa Kabanga Nickel.
Amesisitiza kuwa Tanzania ni sehemu salama na yenye mazingira rafiki kwa uwekezaji katika sekta mbalimbali, ikiwemo Sekta ya Madini ambako amewakaribisha wawekezaji kutoka Australia kuja kuwekeza nchini, huku akibainisha fursa lukuki zilizopo.
Dkt. Kiruswa amesema kuwa, Tanzania inajivunia utulivu wa kisiasa, usalama wa ndani, na Sera thabiti za uwekezaji zinazotoa uhakika kwa wawekezaji huku akiwahakikishia Wawekezaji hao kutoka Australia kuwa Serikali ya Tanzania imeweka mazingira rafiki kwa Wawekezaji wote kupitia Sheria na Kanuni zinazohamasisha maendeleo ya miradi mikubwa ikiwemo ya Sekta ya Madini.
Amesema kuwa, Serikali ya Tanzania imeunda Timu ya Serikali ya Maridhiano, kwa lengo la kuhakikisha uwekezaji unakuwa endelevu na wenye manufaa kwa pande zote, ambako timu hiyo inajumuisha wataalamu wa idara zote kama Sheria, Madini, Kodi, Ardhi, Mazingira na Uchumi ili kuhakikisha masuala yote ya uwekezaji yanashughulikiwa kwa haraka na kwa uwazi na kwamba timu hiyo pia inajumuisha maofisa wanaowasiliana moja kwa moja na wawekezaji ili kutoa mwongozo na msaada kila inapohitajika.
Aidha, Dkt. Kiruswa ameeleza kuwa, Tanzania inakubalika kimataifa kama moja ya nchi zenye utajiri mkubwa wa madini, na kwamba kuna fursa ya kufanya utafiti wa kina wa madini na kwamba Wawekezaji wente nia ya kuwekeza katika Sekta ya Madini wanakaribishwa kuwekeza sambamba na kufanya utafiti wa kina wa kijiolojia.
Kwa kutambua umuhimu wa kuongeza thamani madini ndani ya nchi, Dkt. Kiruswa aamesisitiza kuwa Tanzania imelenga kuanzisha viwanda vya usafishaji na uzalishaji wa bidhaa za madini yanayochimbwa hapa nchiji, hatua ambayo si itaongeza mapato ya taifa pekee, bali pia itatoa ajira zaidi kwa Watanzania na kuchochea maendeleo ya viwanda nchini.
Dkt. Ameongeza kuwa, kwa Sera madhubuti na rasilimali za kipekee, Tanzania inalenga kuwa kitovu cha madini barani Afrika, kwa kuwa Serikali inaweka mazingira bora ya kisheria na kiuchumi ili kuvutia Wawekezaji wakubwa, wa kati na wadogo, sambamba na kuongeza ushawishi wa Tanzania katika masoko ya kimataifa ya madini.
Pia, Dkt. Kiruswa amesema kuwa, ili kuhakikisha Sekta ya Madini inakua kwa ufanisi, Serikali imejikita katika kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani kupitia programu za mafunzo ya kitaalamu na ushirikiano na mataifa mbalimbali ikiwemo Australia kwa lengo la kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na nguvu kazi yenye ujuzi wa hali ya juu itakayosaidia kuendeleza sekta hiyo.
Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Australia hapa nchini, Chris Ellinger amesisitiza kuwa Tanzania ni moja ya nchi inayowavutia Wawekezaji wakubwa kutoka Australia kutokana na uwepo wa fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini na kwamba Tanzania inaendelea kujipambanua kama kitovu cha uwekezaji wa madini kwa miaka ya hivi karibuni.
No comments