#KAZIINAONGEA

DKT. Samia Suluhu Hassan ni mama anayejali maendeleo ya nchi yake sambamba na afya za Wananchi wake, ikiwa ni kwa kuhakikisha miundombinu ya Afya inaboreshwa pamoja na wepesi wa upatikanaji wa huduma muhimu za Kibingwa hapa nchini.

Katika harakati zake za kuboresha Sekta ya Afya kwa kushirikiana na Wataalamu mbalimbali kutoka nje ya nchi, Dkt. Samia ameazimia kutafuta suluhisho la tatizo la figo ambalo limetajwa kuwa miongoni kwa magonjwa hatari na yanayopoteza idadi kubwa ya maisha ya Watanzania hapa nchini.

Tatizo la figo limekuwa likiongezeka siku hadi siku na hivyo kufanya idadi ya watu wenye matatizo ya figo wanaopata huduma ya usafishaji wa damu katika vituo 47 vinavyotoa huduma hiyo hapa nchini, kuongezeka kutoka 1,017 mwaka 2019 hadi kufikia 3,231 Desemba, 2023.

Matunda ya jitihada za Rais. Dkt. Samia yameonekana baada ya Wataalamu wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa kushirikiana na Wataalamu kutoka Shirika la ZGT Overzee la Uholanzi, kufanikiwa kuvuna figo kwa mtu bila kufanya upasuaji, linalojulikana kitaalam kama Laparoscopic Nephrectomy ili kwenda kuipandiza kwa mgonjwa wa figo.

Hii ni mara ya kwanza kwa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kuvuna figo pasipo upasuaji kutoka kwa mtu ambae anamchangia figo ndugu yake mwenye matatizo ya figo tangu BMH ilipoanzisha huduma ya upandikizaji figo, miaka sita iliyopita.

BMH ilikuwa Hospitali ya pili ya Umma kuanzisha huduma ya upandikizaji figo mwaka 2018.

Aina hiyo ya matibabu ya Laparoscopic Nephrectomy, imefanyika hospitalini hapo kwenye kambi Maalumu ya matibabu ya Madaktari Bingwa wa BMH wanaoshirikiana na Madaktari Bingwa kutoka Uholanzi ambao watakuwepo nchini hadi Novemba 16, 2024.

Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof. Abel Makubi amesema kuwa, huduma hiyo hauhusishi kumfanyia upasuaji mtu anaemchangia mgonjwa wa figo, badala yake figo inatolewa kupitia kitundu kidogo.

Ametaja faida ya huduma hiyo ni kuondoa changamoto ya mgonjwa kuugua kwa muda mrefu au kulazwa kwa muda mrefu kwa kuwa, kidonda kinapona haraka.

Faida nyingine ni kupunguza gharama za dawa nyingi kutumika kwa mgonjwa wakati anapatiwa matitabu hospitalini hapo.

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa asilimia 7-14 ya Watanzania ambao ni sawa na watu 10 kati ya 100 nchini wana matatizo ya figo na baadhi yao wanahitaji huduma ya kusafisha damu, huduma ambayo ni ghali sana kulingana na kipato cha Mtanzania.

Gharama za matibabu kwa mgonjwa mwenye matatizo ya figo ni kati ya Shilingi Milioni 31 hadi Milioni 46.8 kwa mwaka mmoja bila kujumuisha gharama za vipimo na usafiri kwa mgonjwa na wasindikizaji wa mgonjwa.

Inakadiriwa kuwa, watu Milioni 850 Duniani wanasumbuliwa na magonjwa sugu ya figo na kati ya watu Milioni 3.1 hufariki kila mwaka na kuufanya ugonjwa huo kushika nafasi ya nane Ulimwenguni kwa kusababisha vifo.

Kwa mujibu wa Daktari Bingwa wa Magonjwa ya figo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Jonathan Mngumi amesema, watu wenye tatizo hili wanakadiriwa kuishi katika nchi zinazoendelea hususan Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Na kwamba, idadi hiyo imekuwa ikiongezeka kila mwaka ambapo kwa sasa inakadiriwa  kuwa, wastani wa asilimia 7 mpaka 25 wa wakazi wa Afrika, wana matatizo ya tigo ambapo, kiasi hicho ni mara tatu zaidi ya nchi zilizoendelea.

#KAZIINAONGEA