#KAZIINAONGEA

Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Manyara itafungua barabara mpya zenye urefu Km.109 katika Wilaya ya Mbulu, Simanjiro pamoja na Babati  katika mwaka wa fedha 2024/2025.

Kaimu Meneja wa TARURA Mkoa wa Manyara Mhandisi Salim Bwaya ameongea na waandishi wa habari mkoani hapo hivi karibuni na kusema kuwa,

Kilomita 109 za barabara zinaenda kuwanufaisha wananchi na kuwaletea manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa kuwarahisishia kupata huduma za kijamii kwa urahisi. 

“Mwaka huu wa fedha tuna mpango wa kufungua barabara katika wilaya  ya Mbulu (Km. 46), Simanjiro (Km. 41), pamoja na Babati (Km. 22) ambapo itajumuisha ujenzi wa barabara za lami (Km. 11.7), changarawe (Km. 251.4) pamoja na matengenezo ya barabara za udongo (Km. 385) na ujenzi wa vivuko vipatavyo 104," amesema.

Aidha Mhandisi Bwaya amesema kwamba licha ya kufungua kilomita hizo za barabara hali ya mtandao wa barabara katika maeneo mengi katika Mkoa huo ni nzuri kwani unapitika katika kipindi chote cha mwaka.

Amesisitiza kuwa, utekelezaji huo unaendelea kutokana na ongezeko la bajeti katika mkoa huo ambapo kwa sasa bajeti yao imepanda mara tatu kutoka Shilingi bilioni 6.788 mwaka 2021 hadi kufikia Shilingi bilioni 19.7 mwaka 2024/2025

“Hili ni ongezeko kubwa na limetuwezesha kuongeza ubora wa mtandao wetu wa barabara kwani mwaka 2021 tulikuwa na barabara za lami Km. 17 na sasa tuna Km. 33.03, barabara za changarawe kutoka Km. 950 hadi kufikia Km. 1980 na kiwango kinachobaki ni kiwango cha udongo”. Ameongeza.

“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuongezea bajeti mara tatu ya bajeti ya awali na hivyo tumeweza kuongeza madaraja ya mawe kutoka daraja (1) mwaka 2021 hadi kufikia madaraja (10),”.

Pia amesema wameweza kuongeza madaraja madogo na ya kati kutoka 283 hadi 530 vilevile madaraja makubwa yameongezeka kutoka madaraja (2) mwaka 2021 hadi kufikia madaraja (28) kwa mwaka huu wa fedha.

Kwa upande wa mabadiliko ya tabia nchi na utunzaji wa miundombinu ya barabara, Mhandisi Bwaya amesema kwamba wanaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara yanayosababishwa na uharibifu wa miundombinu hasa mifereji, kung’olewa kwa alama za barabara na uvamizi wa hifadhi za barabara kwa shughuli za kiuchumi pamoja na umuhimu wa kupanda miti na kutunza mazingira  na kuacha kufanya shughuli zingine za kibinadamu kwenye hifadhi za misitu na kwenye vyanzo vya maji.

Sambamba na hayo Mhandisi Bwaya ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutunza miundombinu ya barabara kwa kuzingatia  sheria na kanuni zake kwani Serikali inawekeza fedha nyingi  kwenye miundombinu ya barabara hivyo ni wajibu wao kuitunza ili waendelee kunufaika nayo kwa muda mrefu.

Nao Wakazi wa Babati wameishukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia na kusema kuwa, Mkoa huo unapokea mazao mengi kutoka vijijini hivyo kukamilika kwa ujenzi wa madaraja na miundombinu mingine imewanufaisha wananchi wengi na hivyo shughuli za uzalishaji zinaendelea kama kawaida. Amesema Bakari Sanka.

Hadija Shabani naye amesema, "tumefurahi sana kwa ujenzi wa madaraja katika kata hizo kwani makorongo yalikuwa mengi na hivyo msimu wa mvua wanafunzi na watoto walikuwa wakipata shida kuvuka ila kwa sasa imewaokoa na kuwarahisishia usafiri".

Hizi ni moja ya juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha maendeleo ya nchi yanamgusa kila Mtanzania.

*#KAZIINAONGEA*