WaterAid, TGNP NA TAWASANET WAJENGA UWEZO KWA WANAWAKE HANANG’
Taasisi ya WaterAid Tanzania, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), na Mtandao wa Asasi za Kiraia zinazoshughulikia Maji, na Usafi wa Mazingira Tanzania (TAWASANET), wamefanya mafunzo ya kujenga uwezo kwa wanawake viongozi kutoka vijiji nane (8) katika Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Mkoani Manyara.
Mafunzo hayo yanalenga kujenga uwezo kwa viongozi wanawake wanaohudumu kwenye Kamati za zahanati na Vituo vya afya, shule za msingi, Bodi za Sekondari na kamati za Huduma za jamii kwenye Halmashauri za vijiji ili waweze kuweka kipaumbele cha upatikanaji wa rasilimali ili kutatua changamoto za maji na Usafi wa mazingira katika maeneo yao.
WaterAid, TGNP na TAWASANET wanatekeleza kampeni ya Afya ya Mwanamke Sasa ambayo inalenga kujenga uwezo kwa wanawake na wanaume ili kuondoa changamoto za Kijinsia kwa kuzipa kipaumbele wakati wa mipango na bajeti sambamba na kuondoa changamoto za kijinsia ambazo zina wakabili zaidi wanawake.
Akiungungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkuu wa Ushawishi, na Uchechemuzi wa sera kutoka WaterAid, Christina Mhando, alisema kwamba suala la ukosefu wa maji ni suala la wanawake, na ni suala la kijinsia, kwahiyo wanawake wanapaswa kulipa kipaumbele katika majadiliano, au maamuzi ya kupanga vipaumbele vya bajeti. “ …. Hata yanapoibuka magonjwa, waathirika wakubwa ni wanawake ndio maana tunashirikiana na wenzetu hawa kujenga uelewa wa jamii jinsi ambavyo masuala ya maji, afya na usafi wa mazingira unavyoweza kuathiri wanawake, watoto wa kike na wazee sambamba kurasimisha masuala ya kijinsia katika sera, bajeti na mipango yote ya serikali za Mitaa” alisema Mhando.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang, Theresia Irafy, wakati wa kufungua mafunzo hayo alisema kwamba, mafunzo hayo ni muhimu kwa wakati huu ukizingatia kwamba wanawake ndio wahitaji na watumiaji wakubwa wa huduma za maji na endapo watapata uelewa na kusimamia vizuri rasilimali za umma sambamba na miradi iliyojengwa italeta tija na kuwezesha kumtua mwanamke ndoo kichwani.
“Ninashukuru wadau hawa kwa kuja Hanang, tunahitaji sana wadau wanaofanya kazi ya kujenga uelewa kwa jamii na kubadilisha mitazamo hasi kuhusu masuala ya kijinsia, mtawezesha kubadilisha mitazamo ya jamii, lakini pia wanawake wanatakiwa kuwa viongozi wazuri wa kusimamia miradi hii sambamba na kuibua na kuweka vipaumbele vya bajeti vyenye mtazamo wa kijinsia” alisema
Mafunzo hayo pia, yamefungwa na Mwenyekiti wa Halmashauri, Bi. Rose Kamili ambaye alisema kwamba suala la maji na usafi wa mazingira ni suala la kijinsia na linatakiwa kuwekewa mkazo kwa wanawake kulielewa na kulisimamia wenyewe kwasababu ndio kundi linaloathirika zaidi endapo huduma za maji na usafi wa mazingira zitakosekana.
“Sisi Halmashauri, tunaendelea kupambana kuhakikisha tunatatua changamoto za ukosefu wa maji kwa baadhi ya maeneo, lakini tuendelee kuwashukuru wadau wetu WaterAid kwa kuwezesha upatikanaji wa maji safi na salama kwa baadhi ya vijiji hasa kwenye taasisi kama zahanati ambako wanawake wanapata huduma zaidi. WaterAid mmekuwa msaada mkubwa kwa wanawake wa Hanang, tunawashukuru sana…” alisema Kamili.
Mafunzo hayo yamewahusisha wanawake kutoka vijiji nane ambavyo ni Gidamula, Gawidu, Muungano, Dajameda, Laghanga, Wareta, Getak na Bashang, ambapo washiriki wamekubaliana kuhakikisha wanahamasisha wanawake kujitokeza kugombea uongozi katika serikali za Mitaa mwaka huu 2024 ili waweze kuwa kwenye nafasi za maamuzi hasa kuibua miradi ya maendeleo itakayotatua changamoto za Maji, afya na usafi wa mazingira (WASH) katika jamii.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/4hFakdc
No comments