Watanzania Milioni 31.2 Kupiga Kura Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mwaka 2024 - Mhe. Mchengerwa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema jumla ya watanzania 31,282,331 wamejiandikisha kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024, ambao ni sawa na asilimia 94.83 ya lengo la kuandikisha wapiga kura 32,987,579.
Waziri Mchengerwa ametoa takwimu hiyo ya watanzania waliojiandikisha kupiga kura, wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Ofisi Ndogo ya TAMISEMI.
“Watanzania wanaume waliojiandikisha ni 15,236,772 sawa na asilimia 48.71 na wanawake ni 16,045,559 sawa na asilimia 51.29 ambao kwa mujibu wa kanuni na sharia ndio watashiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu,” Mhe. Mchengerwa ameanisha.
Mhe. Mchengerwa amesema, takwimu zinaonesha kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya wananchi waliojitokeza kujiandikisha ikilinganishwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2019 ambapo waliandikishwa wapiga kura 19,681,259 sawa na asilimia 86 ya lengo lililokuwa limewekwa la kuandikisha wapiga kura 22,916,412.
Waziri Mchengerwa ameeleza kuwa, ongezeko la idadi ya wapiga kura limetokana na jitihada za uelimishaji na uhamasishaji katika ngazi zote za muhimu zilizofanywa na Ofisi Rais - TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
No comments