Umoja wa Mataifa wampongeza Rais Samia Kukuza Amani,Haki za Binadamu na Demokrasia
Na Mwandishi Wetu
Hatua ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuja na falsafa ya 4R iliyosaidia kuleta majadiliano, maridhiano na ujenzi mpya wa taifa umeufanya umoja wa Mataifa (UN) kuipongeza Tanzania kwa kukuza Amani, haki za binadamu na demokrasia.
UN pia umeipongeza Tanzania kwa kuendelea kusimamia misingi yake mikuu sambamba na kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hii ni kwa mujibu wa Kaimu Mratibu wa Umoja wa Mataifa Bw. Bryan Schreiner kupitia maaadhimisho ya Miaka 79 ya kuanzishwa kwa UN Oktoba 1945 yaliyofanyika katika ofisi za umoja wa Mataifa Jijini Dar es Salaam.
Bw. Bryan Schreiner pia ameipongeza Tanzania kwa kudumisha uhusiano wa muda mrefu na UN ambao una dhamira ya kujenga na kwamba Tanzania ni mwanachama mtiifu wa chombo hicho cha kimataifa tangu Desemba 14, 1961.
Aidha aliipongeza Tanzania kwa kuendelea kuharakisha utekelezaji wa Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu - SDGs kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote na kutetea usawa wa kijinsia.
Aliipongeza Tanzania kwa kuja na Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya kupikia mpango unaolenga kuhifadhi mazingira kwa kuzuia ukataji miti na uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na upishi usio safi unaohusisha matumizi ya kuni na mkaa.
"Kwa miaka mingi, Tanzania imechangia kikamilifu katika kuunda ajenda ya maendeleo ya kimataifa," alisema Bw Schreiner.
Chini ya mkakati wa nishati safi ya kupikia, Tanzania inalenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia hadi ifikapo 2034 kutoka asilimia 10 ya sasa.
No comments