TUME YAWAPIGA MSASA MAOFISA WA POLISI KUHUSU SHERIA ZA UCHAGUZI
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani akifafanua jambo wakati wa mafunzo ya siku moja kuhusu sharia za uchaguzi kwa Maafisa Wakuu wa Upelelezi wa Wilaya nchini. Mafunzo hayo yamefanyika leo Oktoba 17, 2024 jijini Dodoma. Pamoja nae ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini DCI Ramadhani Kingai.
***********
Na Mwandishi wetu, Dodoma
Maafisa wa Polisi nchini wametakiwa kujenga tabia ya kujikumbusha sheria mbalimbali ikiwemo zinazohusu masuala ya uchaguzi ili kuepuka kuyumbishwa na wanasiasa wanaoamua kupotosha yaliyomo katika sheria hizo kwa maslahi yao binafsi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani wakati akifungua mafunzo ya Wakuu wa Upelelezi wa Wilaya nchini yaliyofanyika leo Oktoba 17, 2024 mkoani Dodoma.
Kailima amesema, mafunzo ya aina hii ni muhimu kwa kipindi hiki ambacho kuna Sheria Mpya mbili zinazosimamia masuala ya Uchaguzi. Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024 na Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya mwaka 2024.
“Katika sheria zote mbili yapo mabadiliko makubwa katika maeneo mbalimbali ambayo ni muhimu sana kwenu kuyafahamu kipindi hiki ambacho uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga unaendelea na mwakani itakuwa ni uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani,” alisema Kailima.
Aliongeza, mafunzo hayo kuhusu sheria za uchaguzi yana umuhimu na maana kubwa katika maandalizi ya zoezi zima na mchakato wa kuelekea chaguzi zilizopo mbele yetu kama Taifa.
“Uelewa wenu kuhusu sheria hizi, utasaidia sana usimamiaji wa sheria na kuchukua hatua za udhibiti wa uvunjifu wa sheria hizo pamoja na sheria zingine ili watakaokiuka sheria hizo waweze kufunguliwa mashtaka ipasavyo na kuwatendea haki kwa kitakachoamuliwa na Mahakama,” alisisitiza Kailima.
Aliendelea kwa kusema kuwa, anaamini kuwa baada ya mada inayohusu sheria za uchaguzi kuwasilishwa wakuu hao wa upepelezi watakuwa mabalozi wa kuhamasisha wananchi kwenda kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura pindi zoezi linapofanyika katika maeneo yao.
Lengo la mafunzo kwa maafisa hayo ni kuwajengea uelewa kuhusu haki za vyama, wananchi na makundi mengine katika vipindi vyote vya uchaguzi, kwa maana kabla ya uchaguzi Mkuu, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Pamoja na masuala ya Sheria za uchaguzi, washiriki hao ambao ni Wakuu wa Upelelezi walipata kujua wajibu wa Jeshi la Polisi wakati wa uchaguzi, Bank Note Security features, utambuzi wa bidhaa bandia na hatimiliki, upelelezi sambamba na utafiti katika mapungufu ya kisheria.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini DCI Ramadhani Kingai (kulia) akifafanua jambo akati wa mafunzo ya siku moja kuhusu sharia za uchaguzi kwa Maafisa Wakuu wa Upelelezi wa Wilaya nchini. Mafunzo hayo yamefanyika leo Oktoba 17, 2024 jijini Dodoma. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani.
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Bw. Selemani Mtibora akiwapitisha katika maeneo muhimu yaliyomo kwenye Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024 na Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya mwaka 2024.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani (kushoto) akizungumza jambo na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini DCI Ramadhani Kingai wakati wa mafunzo ya siku moja kuhusu sheria za uchaguzi kwa Maafisa Wakuu wa Upelelezi wa Wilaya nchini. Mafunzo hayo yamefanyika leo Oktoba 17, 2024 jijini Dodoma.
Washiriki wakifuatilia mada
Washiriki mbalimbali ambao ni Wakuu wa Upelelezi Wilaya na Maofisa wengine mbalimbali wakishiriki katika mijadala kuhusu sheria za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/viQ2whH
No comments