Tume maboresho ya kodi yaingia kazini
*Ni ile iliyoundwa na Rais Samia kufuatia
malalamiko ya muda mrefu ya wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji
*Yakusudia kufanya tathmini kwa kushirikisha
wananchi wengi kuainisha changamoto zilizopo
NA MWANDISHI WETU
Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi imeanza kazi na
sasa iko tayari kushirikiana na kumsikiliza kila mdau ili hatimaye mapendekezo
yatakayowasilishwa kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yaakisi uzoefu na maoni ya
kila mwenye mchango wa kutoa katika kuboresha mfumo wa kodi nchini.
Hayo yamebainishwa leo na Mwenyekiti wa Tume hiyo
Balozi Ombeni Sefue akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuanza kazi kwa
Tume iliyozinduliwa Oktoba 4, 2024 na Rais Dkt. Samia kwa lengo la kutathmini
na kushauri kuhusu maboresho ya kodi nchini.
"Tungependa kupitia kwenu, kuwajulisha
wananchi kuwa Tume imeanza kazi, kama mjuavyo Tume hii imeundwa kufuatia
malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi,
wafanyabiashara na wawekezaji kuhusu kero mbalimbali
zinazotokana na mfumo wa kodi nchini. Kodi ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya
nchi yoyote ile duniani," alisema Balozi Sefue na kuongeza,"Hatudhani
yupo mwananchi ambaye hajui umuhimu wa kodi ambazo hatimaye ndizo hugharamia
kwa kiwango kikubwa maendeleo tunayoyatamani na tunayoyastahili. Tatizo lipo
kwenye changamoto zinazojitokeza katika kukadiria na kulipa kodi, ikiwa ni
pamoja na wingi wa kodi, taratibu za kikodi, usumbufu na uwiano kati ya kodi na
mapato mengine ya Serikali yasiyo ya kikodi,".
Kwamba kwa kuunda tume hiyo Rais ameonesha utashi
wa kisiasa wa kushughulikia changamoto hizo ambapo hatua ya kwanza ni kufanya
tathmini ya kina ya mfumo uliopo ili kuwa na msingi wa kufanya maboresho ambayo
ni wazi yanahitajika.
"Hatimaye, lengo la Serikali ni kuhakikisha
kuwa tunakuwa na mfumo wa ukusanyaji mapato ulio rafiki na rahisi, na
unaozingatia haki, usawa na uwazi. Hivyo, tathmini itakayofanywa itazingatia
maeneo yote muhimu ikiwemo Sera, Sheria, Kanuni na taratibu zote
zinazohusika," aliongeza Balozi Sefue.
Balozi Sefue alisema Tume imekusudia kufanya
tathmini hiyo kwa kushirikisha wananchi wengi iwezekanavyo ili kuainisha
changamoto zilizopo, lakini hasa na muhimu zaidi ni kukusanya mapendekezo
yanayotekelezeka na yatakayosaidia kuongeza mapato ya Serikali lakili kwa njia
iliyo rafiki na rahisi zaidi.
"Tunafahamu kwamba uchumi wa nchi yetu unakua
kwa kiwango kizuri. Mathalani katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, pato
halisi la taifa limekuwa kwa wastani wa asilimia 4.7, huku mapato ya kodi
yakifikia wastani wa asilimia 12.1 ya pato la taifa. Kwa kawaida ungetarajia
kasi ya ukuaji huu wa uchumi iende sambamba na kasi ya ongezeko la mapato ya
Serikali. Kiwango tulichofikia cha asilimia 12.1 ya pato la taifa ni chini ya
asilimia 15 ya pato la taifa inayohitajika katika nchi za Afrika Kusini mwa
Jangwa la Sahara ili kujenga uwezo wa kufikia malengo ya kimataifa ya maendeleo
endelevu," alieleza Balozi Sefue.
Kwamba Serikali imedhsmiria kufikia kiwango hicho
cha asilimia 15 ya pato la Taifa ifikapo mwaka 2026/2027, hatua itakayoongeza
uwezo w nchi kugharamia miradi ya maendeleo na kupunguza kiwango cha utegemezi
wa mikopo na misaada.
Hivyo alisema kuwa wanayo kazi kubwa ya kuongeza
mapato ya Serikali ili kufikia kiwango hicho ikiwemo kwa kupanua wigo wa walipa
kodi, kuziba mianya ya ukwepaji kodi, kuongeza ufanisi kwenye kukusanya mapato
na kwa kuweka mazingira mazuri ya wananchi kuanzisha na kukuza biashara, pamoja
na mazingira mazuri ya uwekezaji kwa ujumla.
No comments