Breaking News

SERIKALI YA SAMIA YATUMIA BILIONI 187 KUSAMBAZA UMEME MTWARA, VIJIJI VYOTE VYAFIKIWA

 


NA MWANDISHI WETU

Ni furaha na nderemo kwa wakazi wa Mkoa wa Mtwara mara baada ya Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kufanikiwa kufikisha umeme katika Vijiji vyote 785 vilivyopo katika Mkoa huo.

Serikali imehitimisha kazi Oktoba 28,2024 ya kuwasha umeme katika kijiji cha Makome A ambacho ndio kijiji pekee kilichokuwa hakina umeme.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuwasha umeme katika Kijiji hicho Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala ameipongeza REA kwa kufanikisha ndoto hiyo.

“Tunapenda kumpongeza sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutoa fedha kwa vipindi tofauti kuhakikisha historia hii inaandikwa. Sasa tuna deni kubwa kama wananchi wa Mtwara kuhakikisha tunatumia umeme huu kujiletea maendeleo yaliyokusudiwa,” amesema.

Kanali Sawala pia amewataka wananchi kuhakikisha wanatunza miundombinu ya umeme kwa kuwa serikali ya Rais Dkt. Samia imetumia gharama kubwa sana kufanikisha miundombinu hiyo kufika katika makazi yao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali (mstaafu), Jacob Kingu ametoa wito kwa wananchi wa vijiji vya Mtwara kutumia kipindi hiki cha mauzo ya korosho kuhakikisha nyumba zao zinafanyiwa maandalizi ya kuingizwa umeme na kuunganisha na umeme huo wa REA ili malengo ya serikali yafikiwe.

“Gharama ya kuunganisha umeme huo ni 27,000 tu, bei nafuu ambayo ni kodi wakati gharama zingine zote serikali imezibeba ili kuwaletea maendeleo wananchi wake.

"Tutumie uwepo wa umeme huu kujieletea maendeleo ya kiuchumi,” amesisitiza Balozi Kingu.

Awali akitoa taarifa kuhusu miradi ya REA katika mkoa huo, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA ambaye pia ni Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Mhandisi Jones Olotu amesema kuwa Wakala kupitia miradi mbalimbali iliyogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 187 imewezesha vijiji vyote 785 kupata umeme.

Mhandisi Olotu ameongeza pia baada ya kukamilika kupeleka umeme katika vijiji sasa wakala umeanza safari ya kupeleka umeme katika Vitongoji na kuwahamasisha wananchi kuendelea kutumia umeme huo kujiletea maendeleo

No comments