Breaking News

RAIS SAMIA APONGEZWA KWA KUONDOA VIKWAZO VYA BIASHARA

 


#KAZI INAONGEA

Uwanja wa kufanyabiashara nchini Tanzania sasa uko huru kwa wenyeji na wageni wenye miraji, vikwazo vimeondolewa na ulipaji kodi sasa ni rafiki si wa mabavu.

Hatua hii imefikiwa na uamuzi sahihi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kutaka kuhakikisha Tanzania inaongeza wigo wa uzalishaji mali, kuongeza ajira na kupunguza umasikini.

Ukweli wa hili umewakuna wajumbe wa Bunge la Afrika (PAP) ambao Oktoba 29,2024 wametoa pongezi kwa  Rais Dkt. Samia na Serikali ya Tanzania kwa ujumla kwa kuondoa vikwazo vya biashara kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika kufikia eneo la Biashara Huru Bara la Afrika (AfCFTA) .

Pongezi hizo zimetolewa na wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na kiongozi wa ujumbe wa Bunge la PAP, Profesa Margaret Kamar wakati walipotembelea Kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani (OSBP) eneo la Namanga wilayani Longido mkoani Arusha.

Profesa Kamar amesema katika ziara hiyo wamefika nchini Tanzania kujionea jinsi ya utoaji wa huduma katika maeneo mbalimbali ya mipakani na kwa upande wa mpaka wa Namanga wamejionea jinsi nchi ya Tanzania inavyojitahidi kuhakikisha suala la usalama mipakani linaimarika ikiwemo utoaji na uingizwaji wa mizigo kupitia mashine za kisasa za ukaguzi.

Amesema ajenda kubwa ya Mabunge hayo ni kuhakikisha biashara huru zinaimarika maeneo ya mipakani na wamejionea kwa macho yao juu ya biashara hizo na hatua zinazostahili katika ukaguzi mzuri unaofanywa katika eneo hilo la mpaka wa Namanga.

#KAZI INAONGEA

No comments