Rais Samia achangia milioni 50 kufanikisha ujenzi wa shule ya Msingi na umaliziaji wa majengo Zahanati inayomilikiwa na Bakwata Simiyu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amechangia kiasi cha shilingi milioni 50, katika harambee ya kuchangia ujenzi wa shule ya msingi na umaliziaji wa majengo ya zahanati inayomilikiwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania - BAKWATA mkoa wa Simiyu.
Harambee hiyo iliyoendeshwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa imewezesha kukusanywa kwa shilingi milioni 150 ikiwa ni ongezeko la shilingi milioni 20 zaidi ya shilingi milioni 130 iliyolengwa.
Harambee hiyo imefanyika usiku wa Oktoba 12, 2024, katika adhimisho la Maulid ya Mkoa wa Simiyu kwa mwaka 2024, katika viwanja vya CCM wilayani Bariadi Mkoani Simiyu.
Akizungumza katika harambee hiyo Waziri Mchengerwa aliyepewa heshima ya kuwa mgeni rasmi katika adhimisho hilo la siku takatifu ya kuzaliwa kwa mtume, amesisitiza umuhimu wa elimu dunia na elimu ya dini kwa jamii, akisema elimu ndiyo silaha na nuru ya kujikomboa dhidi ya majanga yote anayokabiliana nayo mwanadamu Pamoja na kupata utukufu.
Kulikazia hilo Waziri Mchengerwa ameiomba BAKWATA iweke miongozo itakayo wajenga waumini katika kusimamia kikamilifu Uzalendo, maadili na kuipenda dini, watu na nchi yao, kuanzia ngazi ya awali, na kusisitiza jamii na wadau mbalimbali wausishwe, watoa mafunzo waanishwe na wajengewe uelewa na uwezo wa maarifa na mbinu kwa maeneo ya vijijini na mjini.
No comments