NISHATI SAFI YA KUPIKIA ITAONDOA KADHIA ZA KUNI NA MKAA KWA WATU WENYE MAHITAJI MAALUM- NDERIANANGA
>Aiasa jamii kuwa na mtazamo chanya juu ya Nishati Safi ya Kupikia
>Asema viongozi wataendelea kuhamasisha Nishati Safi ya Kupikia
Naibu Waziri Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga amesema kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yanaenda kuwaokoa watu wenye mahitaji maalum na kadhia zinazotokana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia ikiwemo kuni na mkaa.
Amesema kadhia hizo wanazipata nyakati za utafutaji na utumiaji wa nishati hizo zisizo safi za kupikia ambazo hutoa moshi mwingi unaoleta pia athari kwenye mfumo wa upumuaji.
Nderiananga ameyasema hayo jijini Dodoma wakati alipokuwa akihamasisha wananchi kupika kisasa kwa kutumia nishati safi ya kupikia kupitia programu ya Pika Kisasa inayoendeshwa na Wizara ya Nishati.
"Natoa rai kwa jamii kuwa na mtazamo chanya juu ya nishati safi ya kupikia ili kuongeza kasi ya matumizi ya nishati hii nchini." Amesema Nderiananga
Ameongeza kuwa, Viongozi katika ngazi mbalimbali nchini wataendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa vitendo na hii inajumuisha Wabunge wanawake nchini kuwa na programu maalum ya kuelimisha jamii majimboni.
Akizungumzia mazingira,amesema faida mojawapo ya nishati safi ya kupikia ni uhifadhi wa mazingira utakaopelekea mvua kupatikana kwa wakati.
Ametaja faida nyingine ya matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kuwa ni jamii kuondokana na magonjwa yanayotokana na matumizi ya nishati isiyo safi ikiwemo athari katika mapafu inayopelekea tatizo la upumuaji.
No comments