Kongamano la Jotoardhi Afrika kuleta uwekezaji na ubunifu mpya Tanzania - Waziri Kaduara
WAZIRI wa Maji, Nishati na Madini wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Shaibu Kaduara amesema Kongamano la Kimataifa la Jotoardhi Afrika (ARGeo-C10) lililofanyika nchini kuanzia tarehe 21 Oktoba 2024 litaleta uwekezaji na ubunifu mpya katika uendelezaji wa nishati ya Jotoardhi Tanzania.
Amesema hayo wakati hafla ya ufungaji wa kongamano hilo iliyofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 25 Oktoba, 2024.
“Maarifa na utaalam uliopatikana katika kongamano hili utasaidia mustakabali wa Tanzania na Afrika katika kufikia suluhisho la upatikanaji wa nishati safi, kuongeza kasi ya maendeleo ya jotoardhi Tanzania na kuongeza mchango wa nishati jadidifu katika uzalishaji umeme.” Amesema Kaduara
Amesema Tanzania imepata heshima kubwa baada ya kuandaa kongamano hilo kwa mafanikio na imekuwa ni fursa ya kutangaza maeneo yake yanayohitaji uendelezaji ikiwemo eneo la Ngozi mkoani Mbeya ambapo kunachimbwa visima vitatu vya uhakiki wa mashapo ya Jotoardhi.
Ameongeza kuwa, kwa kuandaa kongamano la ARGeo-C10 Tanzania imeonesha kwa vitendo nia yake ya kuendeleza jotoardhi, kushiriki katika biashara ya hewa ukaa na kutokuwa na uzalishaji wa hewa ya ukaa.
Waziri Kaduara ametumia fursa ya kongamano hilo kuwasihi Washirika wa Maendeleo duniani kuendelea kuunga mkono jitihada za kukuza nishati ya Jotoardhi barani Afrika.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio, amesema Kongamano la ARGeo-C10 limefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani Nchi 14 ambazo ni Wanachama wa Shirikisho la Jotoardhi Afrika zimeshiriki pamoja na nchi nyinginezo zipatazo 12.
Ameongeza kuwa Kongamano pia limehusisha Wataalam wabobezi kutoka mataifa hayo 26 ambao wametoa mafunzo maalum katika Jotoardhi ikiwemo masuala ya tathmini ya Jotoardhi na jinsi nishati hiyo itakavyosaidia kuangalia masoko ya hewa ya ukaa.
Amesema kupitia Kongamano hilo nchi nyingi zimeonesha nia ya kuwekeza Tanzania baada ya kuona utajiri wa jotoardhi uliopo na utayari wake katika kushirikiana na nchi nyingine duniani ili kuiendeleza.
Amesema nchi nyingi Afrika bado hazijatumia nishati hiyo ipasavyo hivyo Kongamano la ARGeo-C10 limelenga kuharakisha uendelezaji nishati ya Jotoardhi Afrika ili iwe na mchango mkubwa katika gridi za umeme kama ilivyo kwa vyanzo vingine kama vile maji.
Mwakilishi wa Spika la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Joseph Mhagama amesema kongamano hilo la Jotoardhi limewawezesha Wabunge walioshiriki kupata uelewa kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo matumizi ya moja kwa moja ya Jotoardhi, fursa, changamoto na biashara ya hewa ukaa hivyo uelewa huo utawasaidia kutoa ushauri kwa Serikali na kuisimamia Sekta ya Jotoardhi kwa ujumla.
Naye, Mkuu wa Ofisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira Duniani (UNEP) katika nchi za Kusini mwa Afrika, Meseret Teklemarian ameshukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendesha kongamano la ARGeo-10 kwa mafanikio makubwa huku likipewa msukumo mkubwa na Serikali na kwamba UNEP itaendelea kuunga mkono Tanzania kwa namna mbalimbali ili kuendeleza nishati ya Jotoardhi.
Dkt. Peter Omenda, Rais wa Shirikisho la Jotoardhi Afrika (AGA), naye ameishukuru Tanzania kwa kuendesha kongamano hilo kwa mafaniko na kueleza kuwa ni kongamano bora linalopaswa kuigwa na nchi nyingine Afrika.
Ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kujitoa ipasavyo katika kuhakikisha kuwa Kongamano hilo linafanikiwa huku likiwa na washiriki wengi zaidi kuliko makongamano mengine yaliyopita.
Aidha ameeleza kuwa, Kongamano linalofuata litafanyika Comoro mwaka 2026.
Awali, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mathew Mwangomba alisema ARGeo-C10 imeacha alama na kumbukumbu barani Afrika ambapo ameishukuru Serikali na wadau kwa kuwezesha kongamano hilo kufanyika kwa mafanikio.
Amesema Tanzania ipo tayari kushirikiana na wadau wengine ili kuendelea Jotoardhi kupitia utaalam na uwekezaji kwenye maeneo yenye mashapo ya Jotoardhi.
No comments