BRELA yatakiwa kwenda sambamba na maboresho ya Teknolojia ili kukidhi huduma bora na wezeshi.
NA ABRAHAM NTAMBARA
NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe ameutaka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kutobweteka na maboresho ya kimfumo uliofanya bali kuweka mkakati wa kuhakikisha unakwenda sambamba na maboresho ya Kiteknolojia ili huduma yake izidi kuwa bora na wezeshi.
Kauli hiyo Naibu Waziri Kihage ameitoa leo Oktoba 25, 2024 jijini Dar es Salaam akifungua Mkutano wa Pili wa BRELA na wadau wake uliokuwa na lengo la kujadiliana fursa, mafanikio na changamoto zinazoikabili sekta ya biashara hususani katika eneo la Sajili na Leseni za Biashara ambapo BRELA ndiyo lango la uanzishaji wa biashara nchini.
"Nafahamu kwamba kuanzia mwaka 2018 BRELA imekuwa ikitoa huduma zake za Sajili na Leseni kwa njia ya mtandao kupitia mifumo ya Usajili kwa njia ya Mtandao (Online Registration System) na Dirisha la Taifa la Biashara (Tanzania National Business Portal). Mifumo hii imepunguza muda, gharama na bughudha kwa Wawekezaji na Wafanyabiashara ambao walikuwa wanasafiri umbali mrefu kufika katika Ofisi za BRELA Dar es Salaam kwa ajili ya kupata huduma hizo," amesema Naibu Waziri Kigahe na kuongeza,
"Utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao umerahisisha mambo ambapo wafanyabiashara wanaweza kuomba kusajili au kupata Leseni za Biashara zao wakiwa maofisini kwao na wakapata cheti cha Usajili au Leseni pale pale alipo bila kuhitaji kufika katika ofisi za BRELA. Hata hivyo, nitoe rai kwa BRELA wasibweteke na maboresho haya ya kimfumo kwani Teknolojia inabadilika kila siku, hivyo muweke mkakati wa kuhakikisha mnakwenda sambamba na maboresho ya Kiteknolojia ili huduma yenu izidi kuwa bora na wezeshi,".
Akizungumzia kuhusu mkutano huo, Naibu Waziri Kigahe ameipongeza BRELA kwa kuandaa na kuratibu Mkutano huu, lakini pia, amewapongeza wadau wote wa BRELA (Taasisi za Serikali, Sekta Binafsi, Wawekezaji, Wafanyabiashara, Taasisi za Fedha, Wajasiriamali, Vyombo mbalimbali vya habari) kwa kutenga muda na kwenda kushiriki katika mkutano huo ambao ni muhimu katika uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara nchini.
Naibu Waziri Kigahe amebainisha kuwa nafahamu kwamba hii ni mara ya pili kwa BRELA kuandaa tukio hilo ambalo ni tukio muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), kuweza kujitathmini katika utoaji wa huduma, kupokea maoni ya wadau na kutoa majibu pale inapobidi na kuchukua yale mapungufu kwa ajili ya kuyafanyia kazi ili kuimarisha ufanisi wa Taasisi katika kuwahudumia wadau wake.
"Niwapongeze tena BRELA kwa kuandaa na kuwa na utaratibu huu kila mwaka. Katika kipindi hiki, tangu BRELA walipoandaa Mkutano wa kwanza na sasa, naamini kuwa kuna maboresho mengi yamefanywa na BRELA kama Wakala ya Serikali chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ili kuongeza ufanisi na ubora wa huduma zake. Nitoe rai kwa Taasisi zingine za Serikali ambazo hazina utaratibu huu, kuweza kuiga mfano huu mzuri ili kuweza kujipima kwa kupata maoni na mtazamo kutoka kwa wadau badala ya kujifungia na kujitathmini wenyewe maofisini," ameeleza Naibu Waziri Kigahe.
Kwamba BRELA ndiyo lango la urasimishaji wa biashara ambapo usajili wa Makampuni, Majina ya Biashara, Alama za Biashara na Huduma na Leseni za Viwanda husajiliwa.
Ameongeza, pia, BRELA inahusika na utoaji wa Hataza, Leseni za Viwanda pamoja na Leseni za Biashara zenye sura ya Kitaifa na Kimataifa na kwamba kwa kuzingatia majukumu haya muhimu kwa nchi yetu, ni kuwa ufanisi wa utendaji kazi wa BRELA ni muhimu katika ujenzi wa uchumi wa nchi kwani ndipo mahala ambapo biashara zinazaliwa na kuanzishwa.
Hivyo amesema BRELA haiwezi kufanikiwa katika kutekeleza majukumu yake ikiwa peke yake, inategemea ushirikiano na ukaribu na Sekta za Umma na Sekta Binafsi na ndiyo maana Mkutano huo ni muhimu kufanyika ili kufanya tathmini ya wapi BRELA imetoka, ilipo sasa na wapi inaelekea ukizingatia nafasi yake katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa.
Ameeleza matarajio yake ni kuwa Mkutano huo ni nyenzo muhimu katika kuifanya BRELA kuwa taasisi bora na ya mfano katika kutoa huduma bora za sajili na leseni, kutoa elimu kwa jamii ya wafanyabiashara na wawekezaji ili uwekezaji na biashara zinazofanyika ziwe na tija, faida zipatikane kwa wafanyabiashara na Serikali ikusanye kodi kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo na uchumi wa nchi uweze kukua na kuimarika.
Aidha, ametaka Mkutano huo huo uwe chachu kwenu washiriki na muweze kusambaza elimu kwa Wananchi ambao hawajapata fursa ya kuwepo mahali hapa kwani uelewa wao utapunguza kero mbalimbali na gharama za urasimishaji biashara zitapungua na hatimaye mazingira ya biashara nchini kuwa bora na wezeshi.
Alieleza kuvutiwa na Kauli Mbiu ya Mkutano wa Mwaka huu “Mifumo ya Kitaasisi inayosomana na Uwezeshaji wa Biashara nchini” (Interoperability of Institutional Systems and Business Facilitation).
kwamba kauli Mbiu hiyo inalenga kuleta mjadala mpana wa Mifumo ya Kitaasisi kusomana kwa lengo la kutoa huduma zote kwa njia ya mifumo. Mtakumbuka kuwa Serikali ilishatoa maelekezo kwamba ifikapo Mwezi Desemba, 2024, Taasisi za Serikali ziwe na mifumo inayosoamana. Maelekezo haya pia, yalizingatia kuondoa usumbufu na kero zisizo za msingi kwa Sekta Binafsi kwa kuombwa nyaraka hizo hizo kwenye Taasisi mbalimbali za Serikali, wakati nyaraka hizi zingeweza kupatikana kwa njia za mifumo.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Godfrey Nyaisa amesema kuwa mkutano huu wa Pili wa BRELA na wadau wake ulikuwa na washiriki kutoka Sekta za Umma kwa maana ya Wizara mbalimbali, Taasisi na Mashirika ya Umma. pamoja na ushiriki wa Sekta Binafsi zenye mashirikisho yenye wanachama wengi, Wawekezaji, Wamiliki wa Viwanda, Wafanyabiashara, Wajasiriamali, Wabunifu, Ofisi za Mawakili na wafanyabiashara wadogo kabisa. Mchanganyiko huu wa washiriki kutoka Sekta za Umma na Sekta Binafsi utaleta majadiliano yenye tija kwa manufaa ya pande zote mbili.
No comments