BRELA kukutana na wadau kujadili fursa, mafanikio na changamoto zinazowakabili
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Godfrey Nyaisa akifafanua jambo.
NA MWANDISHI WETU
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imeandaa Mkutano wa Pili wa BRELA na Wadau wake, utakaofanyika Oktoba 25, 2024 kuanzia saa 1.30 asubuhi mpaka saa 10.30 jioni, katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Oktoba 23, 2024 jijini Dar es Salaam na Kitengo cha Habari na Mawasiliano BRELA, mkutano huo ni wa pili kufanyika ambapo utawakutanisha wadau mbalimbali kutoka Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.
Kwamba lengo ni kujadili fursa, mafanikio na changamoto zinazowakabili wadau wa BRELA na Sekta ya Biashara kwa ujumla.
Taarifa hiyo imeeleza, pia, mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano baina ya BRELA na wadau wake kutoka Sekta ya Umma na Binafsi ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu huduma zinazotolewa na BRELA na Taasizi zingine zinazoratibu urasimishaji wa biashara nchini.
"Kauli mbiu ya Mkutano huu ni “Mifumo ya Kitaasisi inayosomana na Uwezeshaji wa Biashara nchini” (Interoperability of Institutional Systems and Business Facilitation)," imeeleza taarifa hiyo na kuongeza,
"Kauli mbiu inakwenda sambamba na maagizo na maelekezo ya Serikali ya kuhakikisha mifumo inasomana ifikapo Mwezi Desemba mwaka huu. Pia, kwa kuwa urasimishaji wa biashara ni mchakato, ni vema kupitia Mkutano huu Sekta za Umma zinazoratibu urasimishaji wa Biashara nchini wakasikiliza namna bora ya Sekta Binafsi inavyopenda ihudumiwe kupitia mifumo kusomana,".
Kwamba kutokana na uzoefu uliopatikana katika Mkutano wa kwanza wa wadau wa BRELA uliofanyika Oktoba 27, 2023 na kuhudhuriwa na washiriki wapatao 350, ulitoa mwanga na kuonesha umuhimu wa kukutana na kukaa pamoja na wadau kila mwaka, ili kubaini fursa, mafanikio na changamoto wanazokabiliana nazo sekta binafsi.
"Mikutano kama hii kwa kiasi kikubwa inasaidia kupata uelewa wa pamoja kuhusu namna ya kupata majawabu ya fursa, mafanikio na changamoto. Inatarajiwa katika Mkutano huu, wadau wataweza kupata mrejesho wa majukumu yanayofanywa na BRELA," imebainisha taarifa hiyo
Hivyo watapata mrejesho wa maoni, ushauri na mapendekezo ya wadau kwenye Mkutano wa BRELA na Wadau wake uliofanyika mwaka jana.
Kadhalika kujadili mada kuhusu mifumo ya Taasisi za Serikali kusoma na uwezeshaji kibishara nchini.
Vile vile kupata mrejesho wa huduma za BRELA na kuweka mkakati wa pamoja ili kuboresha huduma zinazotolewa na kupata maoni juu ya utendaji kazi wa BRELA hasa matumizi ya mifumo kwa kusomana na mifumo ya Taasisi zingine.
Pia, kubaini changamoto zinazowakabili wadau na kuzitafutia ufumbuzi ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini na kukuza uelewa wa wadau kuhusu sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza utoaji wa huduma za usajili na ulinzi na utoaji Leseni ili kuimarisha utekelezaji wa sheria za nchi.
Sambamba na Kujadili masuala yanayohusu maendeleo ya Sekta ya Biashara nchini ikiwemo fursa zinazotokana na mabadiliko ya teknolojia na namna yanavyochochea ukuaji wa biashara.
Mkutano huo wa Pili wa BRELA na Wadau wake utawakutanisha wadau zaidi ya 300, wakiwemo wawakilishi wa taasisi za umma, sekta binafsi, Taasisi miamvuli, wafanyabiashara, wanazuoni, wajasiriamali na Mawakili kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini.
Vile vile mkutano huu pia, utakuwa sehemu ya kubadilishana uzoefu utakaowezesha kuboresha na kuimarisha huduma pamoja na kuongeza ufanisi na tija kwenye utoaji wa huduma na utasaidia kutatua changamoto wanazokutana nazo wateja na wadau wa BRELA.
Mkutano huu utaendeshwa kwa muundo wa Mdahalo ambao utawezesha watoa mada, wachagizaji na waongoza mijadala kuhusiana na mada zilizopo kuibua mjadala kulingana na mada husika pamoja na kauli mbiu ya Mkutano huu wa pili.
Kwamba kauli mbiu hii, itatumika katika kuakisi mada zitakazo tolewa kwa kuzingatia ushiriki wa wadau waliopo kwenye mnyororo mzima wa urasimishaji na ufanyaji wa biashara nchini. Washiriki wapatao 300 wanatarajiwa kushiriki katika Mkutano huu ambapo Taasisi mbalimbali zimeonesha nia ya kushiriki katika Mkutano kama washiriki na baadhi wakiwa sehemu ya wadhamini. “Tunaipa uhai wa kisheria biashara yako”.
No comments