ATLAS SCHOOLS MARATHON 2024 kuunga mkono Serikali kutokomeza ukatili kwa watoto.
NA MWANDISHI WETU
UONGOZI wa Shule za Atlas Primary School Madale, Ubungo na Atlas Sekondary Madale pamoja na Kamati ya Maandalizi ya Siku ya Atlas (Atlas Day) umesema Atlas Schools Half Marathon 2024, itafanyika Oktoba 14 mwaka huu na kwamba lengo kuu la mbio hii ni kuungana na Serikali kuboresha usalama wa watoto na pia kutokomeza ukatili dhidi ya watoto.
Hayo yamebainishwa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Siku ya Atlas (Atlas Day) Mwalimu Willbroad Prosper akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu siku hiyo inayojumuisha Atlas Schools Half Marathon, Mahafali, Maonyesho ya vitu mbalimbali, michezo ya watoto na burudani ambayo itafanyika Oktoba 14, 2024 katika viwanja vya Atlas Schools Madale.
"Tutaanza kuanzia saa 11:00 Alfajiri kwa mbio yaani Atlas Schools Half Marathon na baadae kufuatiwa na Mahafali yatakayoanza kuanzia saa 4:00 Asubuhi na kuendelea pamoja na uwepo wa matukio mbali mbali. Katika Siku hiyo (Atlas Day) tutaanza na Atlas Schools Half Marathon ambapo tutakua na mbio za 21km, 10km na 5km) ambazo mbio hizi zitaanzia hapa hapa katika viwanja vya shule za Atlas Madale na kuhitimishwa hapa hapa (Yaani starting na Finishing Point ni hapa hapa shuleni)," alisema Mwalimu Prosper na kuongeza,
"Lengo kuu la kuwa na mbio hizi kwa mwaka huu ni kuungana na Serikali kuboresha usalama wa watoto na pia kutokomeza ukatili dhidi ya watoto kama kauli mbiu yetu kwa mwaka huu inavyosema “Run for Wellness, Good health for our future generation” Vile vile kwa mwaka huu ambapo tarehe ya kufanyika kwa mbio yetu imeangukia siku ya kumbukizi ya Baba wa Taifa Mwl. JK Nyerere tarehe 14/10/2024 na kama ilivyo ada kwa miaka ya nyuma basi tutakua tukisherehekea kumbukizi ya Baba wa Taifa Mwalimu Julias Kambarage Nyerere,".
Hivyo alisema kwa kuenzi kazi nzuri alizozifanya katika Taifa kwa mwaka huu Marathon hiyo itakuwa na mambo mengi ambayo yataendana na yale mazuri aliyoyatekeleza kipindi cha uhai wake.
"Kwa wale wote watakaopenda kushiriki mbio hizi kwa 5km, 10km na 21km basi mnakaribishwa na utachangia ada kidogo tu ya ushiriki ambayo ni Tshs 35,000 kwa mtu mmoja, na kwa kikundi cha watu wasiopungua 20 basi watapata punguzo la asilimia 10 hivyo basi watachangia Tshs 31,500 tu. Baada ya kujisajili, mshiriki atapata Fulana ya kukimbilia, Namba ya kukimbilia (bib number), na pia njiani atapata huduma zoote muhimu za kukimbia kama vile Maji, Matunda, huduma ya kwanza, wrist band, na atakapomaliza mbio atapatiwa medal nzuri na viburudisho kama vile soup yenye viwango na nyama choma," alieleza Mwalimu Prosper.
Kwamba katika kuhakikisha usalama kwa wakimbiaji, kamati ya maandalizi imejipanga vizuri kabla na baada ya kuanza mbio kwa kupima vizuri umbali wa mbio hizo kwa 5km, 10km na 21km kwa kushirikiana na chama cha riadha Taifa (RT) na pia kuweka vituo vya huduma vya kutosha yaani Water Points, Ulinzi wa uhakika ambao utasimamiwa na Jeshi la Polisi pamoja na SGA Security, Maji ya kutosha ya Kilimanjaro kama navyoyaona hapa, matunda, Juice, na wataalamu mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha mbio hiyo inafana.
Alibainisha kuwa usajili wa mbio hiyo unaendelea katika Shule za Atlas, yaani Atlas Primary School Madale, Atlas Primary School Ubungo na Atlas Secondary School Madale na pia usajili unaendelea Mlimani City ambapo katika maeneo yote hayo, ukisha sajili tu utaondoka na kila kifaa chako cha kukimbilia siku ya Oktoba 14, 2024, lakini pia usajili unafanyika kwa kupitia Lipa namba ya Tigo ni 5927380 Atlas Schools.
Kwamba kwa kujali ushiriki wa wakimbiaji wa aina mbalimbali, kamati ya maandalizi imeandaa zawadi kwa washindi watano kwa jinsia zote kwa mbio za Kiometa 21 (Half Marathon), Kilometa 10 (Social & Corporate Run), na Kilometa 5 kwa watoto (Funrun & Corporate).
Alibainisha kuwa baada ya shughuli ya Marathon kukamilika washiriki wote watapata muda wa kupata burudani kama vile, Soup, nyama choma, maonyesho ya bidhaa mbalimbali, Muziki Mzuri wa Djs, Live band, huduma ya chakula na vinywaji na burudani kemkem kuendelea kwa siku nzima.
Sambamba na hilo, pia kutakua na sherehe za Mahafali ya 19 ya shule za Atlas ambapo wanafuzi zaidi ya 700 watakua wakitunukiwa tunzo baada ya kuhitimu elimu yao ikiwa ni pamoja na wahitimu wa Nursery, Darasa la Saba na Kidato cha nne.
Kwamba wahitimu kutoka katika shule zote tatu Atlas Primary School Ubungo, Atlas Primary School Madale na Atlas Secondary School Madale watasherehekea mahafali pamoja na wazazi wao kwa aina tofauti kwani tunatarajia ushiriki wao katika marathon utachagizwa na tunzo mbalimbali ikiwemo medal ambapo mwanafunzi anaweza kutunukiwa cheti na medal ya kukimbia marathon na ikawa kumbukumbu nzuri kwake na Mzazi wake.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Riadha (RT) Mkoa wa Dar es Salaam Samwel Mwera aliishukuru kwa namna Shule za Atlas zinavyoandaa mbio hizo kwani wamekuwa wakishirikiana hatua kwa hatua na kwamba uongozi wa shule umekuwa ukifuata taratibu zote.
Naye Mjumbe wa Kamati ya Ufundi kutoka Mamlaka za Usajili Riadha Ranzania (RT) Kanda ya Pwani Felix Chunga alisema kwamba Shule za Atlas zimekuwa ni mdau wao mkubwa na wamekuwa wakishitrikiana kwa msimu wa tano sasa.
Alisema kwamba ni wajibu wao kuhakikisha wanasimamia mbio hizo kwa kufuata taratibu na sheria, hivyo wamekuwa wakishirikiana na Shule za Atlas kuboresha mbio hizo.
No comments