NA MWANDISHI WETU
Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dkt. Fredrick Shoo, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anastahili kuongoza vipindi viwili
Dkt. Shoo amewashangaa watu wanaotamani Rais Dkt. Samia aongoze kipindi kimoja.
Katika mahubiri yake kwa waamini wa Kanisa hilo hivi karibuni, Dkt. Shoo amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hahitaji kupigiwa debe kwa njia zisizo faa kwa sababu Mungu amekwisha kumuweka, ni Rais wetu.
"Sio tu kwa kipindi hiki, bali kwa vipindi viwili, mtanishangaa mtasema Askofu Shoo unapiga siasa, hapana, mimi nilioneshwa na niliyasema maneno haya mwanzoni kabisa.
"Wapo waliosema huyu ni mwanamke, nikawaambia hapana, Mungu amepanga iwe hivyo na huyu ndio atakuwa Rais wetu na tutamheshimu.
"Kuna wanaotamani amalizie kipindi hiki, sasa mimi najiuliza kwanini isiwe vipindi viwili?!
"Hawa marais wetu tumeweka historia nzuri, kwa mujibu wa Katiba marais wanakaa vipindi viwili, huyu mnasema aishie kipindi kimoja kwa kuwa ni mwanamke!! Acheni hizo.
"Ndugu zangu ni kwa neema ya Mungu tumepewa Rais huyu na kwa neema hiyo hiyo atahitimisha kipindi hiki cha kwanza na kwa neema hiyo hiyo ataongoza kipindi cha pili."
Tangu aingie madarakani Rais Dkt. Samia amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha anafikisha maendeleo kwenye kila kona ya nchi pamoja na kufungua milango ya maridhiano na kuruhusu haki ya kikatiba ya kutoa maoni kwa wote.
No comments