Breaking News

WAZIRI RIDHIWANI APONGEZA BARAZA LA LESCO KWA UTENDAJI MZURI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhr. Ridhiwani Kikwete akizungumza na Wajumbe wa Baraza la Ushauri wa masuala ya Kazi, Uchumi na Jamii (LESCO), walipokutana jijini Dodoma.

Na: Mwandishi wetu – Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amepongeza Baraza la Ushauri wa Masuala ya Kazi, Uchumi na Kijamii (LESCO) kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yake.

Mhe. Ridhiwani ametoa pongezi hizo leo Septemba 5, 2024 jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na Wajumbe wa Baraza hilo wanaomaliza muda wao.

“Nitumie fursa hii kuwapongeza kwa moyo wa dhati kwa kutekeleza vema majukumu yenu kwa ufanisi ili kuhakikisha malengo ya kuanzishwa LESCO yanatimia” amesema.

Aidha, amesema katika kipindi cha miaka mitatu, LESCO imefanya kazi nzuri ya kuishauri serikali kuhusu sera zinazohusu masuala ya Ajira na Kazi; upangaji wa kima cha chini cha mshahara katika sekta binafsi; Uridhiaji wa mikataba ya Shirika la Kazi Duniani; na ushirikishwaji wa wadau wa Utatu (Serikali, Waajiri na Wafanyakazi) katika masuala ya kazi, Uchumi na jamii.

Ametoa rai kwa wajumbe wa baraza hilo kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuhakikisha sekta ya kazi na ajira inazingatia misingi ya kazi zenye staha kwa maslahi ya wafanyakazi na waajiri.

Awali, Mwenyekiti wa LESCO Dkt. Samwel Nyantahe ameishukuru serikali kwa kutoa ushirikiano katikia kipindi chote cha utekelezaji wa majukumu yao.

Uongozi wa Baraza hilo unamaliza muda wake Septemba 12, 2024 na kwasasa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imeanza mchakato wa kuwapata wajumbe wengine.

No comments