Tarafa ya Ngorongoro wapongezwa kwa kudumisha Amani
Na Hamis Dambaya, NCAA
Serikali imewapongeza wananchi wa tarafa ya Ngorongoro
mkoani Arusha kwa kuendelea kudumisha umoja, amani na utulivu katika eneo hilo
na hivyo kuendeleza falsafa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutaka wananchi wote kuishi kwa
maelewano.
Akizungumza mara baada ya ibada ya shukrani iliyofanyika
katika Kanisa katoliki la Mtakatifu Luka lilipo katika kata ya Endulen wilayani
Ngorongoro mkoani Arusha mshauri wa Rais wa masuala ya siasa na uhusiano wa
jamii balozi Rajab Luhwavi amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefurahishwa na utulivu mkubwa walioonesha
wananchi wa tarafa hiyo na kusema serikali inafuatilia kwa karibu maelekezo
yake yote katika eneo hilo.
Balozi Luhwavi amewataka wananchi hao kuendelea kuwa
wavumilivu wakati serikali katika ngazi mbalimbali ikiendelea kutekeleza
maelekezo ya Mheshimiwa Rais huku akisisitiza umuhimu wa wananchi hao kuendelea
kupendana na kushirikiana na serikali katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (
NCAA) Dkt. Elirehema Doriye aliwaambia wananchi hao kuwa Mamlaka yake
itasimamia na kutekeleza maelekezo yote yanayoihusu mamlaka hiyo yaliyotolewa
na wawakilishi wa mheshimiwa Rais na kwamba hatua mbalimbali zimechukuliwa
katika kutekeleza maelekezo hayo.
Kwa upande wake mbunge wa Ngorongoro Mheshimiwa Emmanuel Ole
Shangai ameipongeza serikali kutokana na kuchukua hatua madhubuti za
kuhakikisha miradi mbalimbali ya maendeleo inatekelezwa na kusema kuwa
ataendelea kusimamia suala hilo ili kuleta maendeleo kwa wakazi wa eneo hilo.
Mheshimiwa Ole Shangai amempongeza Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na upendo
wake mkubwa kwa wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro uliopelekea wananchi wa eneo
hilo kuruhusiwa kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa na kufuta
tangazo lililotolewa la kuvifuta vijiji katika tarafa hiyo.
Mapema Paroko wa kanisa hilo Padri Albano Mwombeki
amewaongoza wananchi hao katika ibada hiyo ya shukranI na kuwataka kuendelea
kudumisha amani,utulivu na mshikamano ili waweze kujiletea maendeleo yao na
taifa kwa ujumla.
No comments