Tanzania Nchi ya mfano Utekelezaji mpango wa ushirikiano Sekta Binafsi Japan na Wakulima wadogo wa Kahawa unaotekelezwa na IFAD
Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kwa ushirikiano
wa Wizara ya Kilimo, Misitu na Uvuvi ya Japan (MAFF) na sekta binafsi chini ya
makampuni makubwa ya Japan yanayojishughulisha na kahawa ya UCC Holdings na Marubeni;
zilizindua utekelezaji wa Mpango wa Ushirikiano kati ya sekta binafsi na wakulima
wadogo wa zao la kahawa ambapo, Tanzania imechaguliwa kuwa nchi ya kwanza na ya
mfano katika utekelezaji wa Mpango huo.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mheshimiwa Balozi Baraka
Luvanda alizihakikishia kampuni za Japan, uwepo wa mazingira wezeshi ya
biashara na hata uwekezaji wanapoamua kuwekeza katika kilimo au sekta
nyinginezo. Amelitaja kuwa zao la kahawa ni miongoni mwa mazao ya kimkakati
nchini ambalo, linatumika kibiashara kwa kulipatia Taifa pato kubwa kwa mauzo
mengi ya kigeni. Akitolea mfano wa Japan, alieleza kuwa kwa mwaka, Tanzania
inauza kahawa yake Japan kwa wastani wa asilimia 34 ya kahawa inayolimwa
nchini, ambayo ni sawa na wastani wa kilogramu million 15 (tani 15,000) ya kahawa
yote ya Tanzania inayouzwa nchini Japan. Takwimu hizo zinaiweka Japan kuwa mnunuzi
mkubwa na namba moja (1) wa kahawa inayolimwa nchini.
Aidha, Balozi Luvanda alielezea juhudi za Serikali ya Awamu
ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kuwa imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo kwa
kuwekeza katika miradi ya muda mrefu na mifupi pamoja na maeneo ya msingi ya
kutatua changamoto za kilimo kuanzia shambani hadi sokoni ili kujihakikishia
uhakika wa chakula, kulisha wengine kibiashara duniani, na pia wakulima
kujipatia kipato cha kutosha ili kupunguza umaskini.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Mitsuo Takahashi, Naibu Waziri
wa Kilimo, Misitu na Uvuvi wa Japan, anayehusika na Masuala ya Bunge la Japan,
katika hotuba yake alieleza kuwa Japan na Tanzania ni washirika wakubwa wa
maendeleo hususan, katika sekta ya kilimo. Alibainisha kuwa Japan inaitambua
Tanzania kwa uzalishaji wa kahawa yenye ubora ambayo, imejizolea umaarufu na
kuwa miongoni mwa kahawa tatu bora nchini humo. Kwa umuhimu huo, alieleza kuwa
Serikali ya Japan kwa kushirikiana na sekta binfasi kupitia makampuni ya
Marubeni na UCC Hodlings imedhamiria kutekeleza Mpango wa ELSP unaoratibiwa na
Shirika la IFAD kuliongezea thamani na uzalishaji zao hilo kwa kuboresha
mazingira ya kilimo kwa wakulima wadogo wa kahawa kusini mwa Tanzania, katika
mikoa ya Mbeya na Ruvuma.
Aidha, Waziri Takahashi, alielezea chimbuko la Mradi huo kuwa mnamo mwezi Aprili 2023, Wizara ya Kilimo, Misitu na Uvuvi (MAFF) ya Japan ilitangaza kuanza utekelezaji wa ‘Mapango wa Ushirikiano kati ya Sekta Binafsi na Wazalishaji Wadogo (ELPS)” ukiwa ni moja ya maazimio yaliyopitishwa na Marais wa Nchi zenye Nguvu Kiuchumi Duniani wa Kundi la G7 kwenye Mkutano wao uliofanyika jijini Hiroshima, Japan.
Vilevile, kwa upande wake Bi. Gerardine Mukeshimana, Makamu
wa Rais wa IFAD, aliuelezea Mpango wa ELPS unaotekelezwa na Shirika hilo, kuwa
unalenga kubadilisha kilimo cha wazalishaji wadogo kwa njia endelevu kwa
kuboresha uzalishaji wao na upatikanaji wa soko kwa kuchochea ushiriki wa sekta
binafsi na uwekezaji katika kilimo na mifumo ya chakula. Alieleza kuwa Mpango
huo una lengo mahsusi katika kuunganisha
wazalishaji wadogo na makampuni ya sekta binafsi, kutumia
mitandao ambayo IFAD imeianzisha katika maeneo ya vijijini kwa nchi
zinazoendelea. Hivyo kufuatia lengo hilo, alifafanua kuwa IFAD, kwa ushirikiano
wa karibu na MAFF na kampuni za UCC na Marubeni, imeanzisha Mradi wa Kwanza wa
Majaribio wa Mpango huo na kuwa nchi iliyochaguliwa ni Tanzania kupitia zao la
kahawa; Mradi huo utasaidia vyama tisa vya ushirika vya wakulima Tanzania
(AMCOS) katika mikoa ya Mbeya na Ruvuma, utakaogharimu takriban Dola za
Marekani 460,000.
Mwishoni mwa mwezi Juni hadi mapema Julai 2024, IFAD pamoja na UCC na Marubeni, zilifanya ziara nchini Tanzania ili kutekeleza Mpango wa ELPS kwa uwekezaji wa pamoja. Tukio la Uzinduzi wa Mpango huo lililofanyika Tokyo, Japan, tarehe 20 Septemba 2024, limelenga kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya wadau hao wakubwa ili kuhakikisha utekelezaji wake unafanikiwa. Pia, kwa upande wa Japan, uzinduzi huo umelenga kuweka Mpango wa ELPS kuwa ni mfano wa kuigwa wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi; na kwa upande wa IFAD, uzinduzi huo umelenga kukuza maslahi na mahitaji miongoni mwa washirika watarajiwa wa sekta binafsi pamoja na Serikali za Kundi la G7 hususan, katika kuujengea uwezo Mpango wa ELPS.
No comments