Breaking News

MWINJILISTI NGEMERA ATANGAZA KUUNDWA KWA DHEHEBU LA WAAFRIKA WOTE


Mwinjilisti Silvanus Ngemera akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

NA MWANDISHI WETU 

MWINJILISTI Silvanus  Ngemera ametangaza kuundwa kwa dhehebu Maalum la Waafrika wote katika Nchi 42 Kusini mwa Sahara linaloitwa African Orthodox Derekh.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 6, 2024 jijini Dar es Salaam Mwinjilisti Ngemera amesema kuwa Derekh ni ndilo jina lililotumiwa na Kanisa la kwanza pale Yerusalemu lenye maana ya NJIA YA MUNGU.

"UKRISTO WA KIAFRIKA ni ule ulioshikamana na Utamaduni chanya wa Mwafrika bila kujumuisha Miungu, Mizimu, Uaguzi, kuloga, Uchawi, Matambiko, Ramli na Dhambi zingine," amesema Mwinjilisti Ngemera.

Akieleza kuhusu sababu za kuundwa dhehebu la Waafrika, amesema Madhehebu yote ya Ukristo Afrika Kusini mwa Sahara ni matawi ya Madhehebu ya Ulaya na Marekani, na kwa jinsi hiyo yanaongozwa Kutoka Ulaya na Marekani.

Kwamba kuongozwa kutokea Ulaya na Marekani unakuwa ni kama "Ukoloni wa Dini" ambao haukukusudiwa na Mungu Wala mjumbe wake, Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi ambapo Ukristo ni kinyume cha Ukoloni.

Amesema kuunda dhehebu Moja kwa Waafrika wote Kutoka Cape Town hadi Juba, hadi Accra na kuyakataa Madhehebu ya kigeni na makanisa binafsi ambapo amebainisha kuwa umoja wa Ukristo wa Waafrika na Wazungu hauna maslahi kwa Waafrika ki-imani na ki-wokovu.

Mwinjilisti huyo ameendelea kueleza kuwa AFRICAN ORTHODOX DEREKH ni taasisi kubwa ya Mungu, isiyomilikiwa na mtu yeyote ambayo inamilikiwa na Mungu na kuongozwa na Mchungaji Yesu na Waamini wote.

"Tukisha kufanya uamuzi huu wa kujitenga kiuendeshaji na Ukristo wa Wazungu na kuchukua upya Ukristo Kutoka kwenye shina lake mjini Yerusalemu kama tunavyoruhusiwa na Bibilia yenyewe, basi tunalazimika pia kuunda upya Teolojia, Katekizimu na Liturujia yetu," ameongenza Mwinjilisti Ngemera na kusema,

"Tunalazimika pia kuondoa uchakachuaji wa Dini uliofanywa na Madhehebu ya kale kwa kujitungia baadhi ya mambo, kuyanyamazia mambo yaliyo muhimu kwa Dini hii, na kuingiza mambo ambayo hayamo kwenye Biblia au hata yanayopigana nayo,".

Amebainisha kuwa dhehebu hilo ni la Mungu, hivyo itamlenga Mungu zaidi katika mafundisho yake ambapo ameeleza kuwa Mungu ni mmoja na wanaikataa hoja potofu ya utatu mtakatifu.

No comments