Breaking News

Waziri Kijaji atoa wito kwa Wananchi kutumia Nishati safi ya kupikia, Asema inamuondolea adha mtoto wa Kike



Na Mwandishi Wetu 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema uwepo wa Nishati Safi ya Kupikia kunamuokoa mtoto kike na athari (adha) zitokanazo na matumizi ya nishati isiyo safi kama kuni na mkaa.

Ametaja athari hizo kuwa ni pamoja na kukosa muda wa kujisomea kwa kwenda kutafuta kuni na magonjwa yatokanayo na nishati isiyo safi.

"Ninaposikia nishati safi ya kupikia  ninaona ni jambo zuri ambalo linakwenda kumuokoa mwanamama, mtoto na hata baba ambaye anahangaika kwa muda mrefu na  utafutaji wa kuni na mkaa na athari za matumizi ambazo ni nishati zisiyo safi na salama" Amesema Dkt. Kijaji

Aidha, amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa mkakati wa nishati  safi ya kupikia barani Afrika, na kuongeza kuwa mkakati huo wa matumizi ya nishati safi na salama unakwenda kuwaondoa watanzania katika kuhangaika kutafuta kuni na hivyo kuutumia muda mwingi kuwekeza kwenye shughuli za maendeleo. 

Ametoa wito kwa wananchi kutumia nishati safi ya kupikia ili kulinda mazingira, ikiwemo vyanzo vya maji ambavyo vipo kwenye misitu pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi  akitolea mfano mvua zisizo tabirika.

Ameongeza kuwa kulinda na kuyatunza mazingira kutasaidia watanzania kuondokana na changamoto za kiafya zinazoambatana na nishati isiyo safi.

"Miti mingine ina sumu ndani yake, wakati wa kupika kwa kutumia mkaa inaweza leta athari na kuna mingine inatoa moshi mama akivuta moshi ina athiri mapafu yake." Amesisitiza Dkt. Kijaji.

No comments