Kafulila: Watanzania anzisheni fursa za uwekezaji
.....awataka kutosubiri tangazo la zabuni za Serikali
....aeleza njia nne Sekta ya Umma, Binafsi zanavyofanya kazi
pamoja
NA MWANDISHI WETU
Mkurugenzi Mtendaji wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi - (PPP)
David Kafulila amewashauri wafanyabiashara na wawekezaji nchini wasisubiri zabuni
ya Serikali itangazwe ili waweze kupata fursa na badala yake wenyewe waanzishe fursa.
Ushauri huo Kafulila aliutoa jana katika mahojiano
maalumu na chombo kimoja cha habari jijini Dar es Salaam akieleza namna Sekta ya
Umma na Sekta Binafsi zinavyoweza kufanya kazi kwa pamoja.
Kamishna Kafulila alieleza kuwa Sheria ya Ubia kati ya Sekta
ya Umma na Sekta Binafsi ina maeneo manne ambayo yanatoa nafasi kwa pande hizo
mbili kuweza kufanya kazi kwa pamoja.
Alisema kuwa njia ya kwanza ni ile ambayo Serikali inahitaji
kufanya mradi kwa utaratibu wa ubia, hivyo inauanda mradi husika kwa maana ya
kufanya upembuzi yakinifu ambapo itaonesha sifa za mradi za kibiashara,
kiuchumi na sifa nyingine.
Kwamba upembuzi huo ukishafanyika, mradi unapelekwa sokoni
kwa maana ya kuutangaza ili kampuni binafsi zishindane na kuchukua fursa hiyo, ambapo
alieleza kuwa njia hiyo Serikali inaanzisha yenyewe mradi na kuuweka sokoni.
“Njia ya pili ni ile ambayo Sekta Binafsi inaona fursa, kwa
mfano inaweza kuwa jinsi ambavyo Serikali inaendesha Reli ya SGR labda kutoka Dar
es Salaam mpaka Dodoma, mwekezaji anaweza kusema, ningepewa mimi kampuni binafsi
ningeweza kufanya vizuri zaidi ya inavyofanya kwa faida yangu na kwa faida ya
Serikali na kwa faida ya umma. Kwa hiyo hii ni ile ambayo Sekta Binafsi yenyewe
imeichungulia fursa. Kimsingi fursa inakuwepo,” alitoa mfano Kamishna Kafulila
na kuongeza,
“Na huu ni ujumbe kwa Watanzania ambao wapo katika masuara ya
biashara na uwekezaji kwamba kwenye masuala ya ubia hauhitaji kusubiri zabuni
ya Serikali itangazwe ili uweze kupata fursa na badala yake wewe mwenyewe unaweza
kuanzisha fursa. Kimsingi fursa inakuwepo,”.
Alieleza kuwa ili kuanzisha fursa hiyo ni kupeleka kusudio la
kuwekeza katika eneo kulani ambalo mamlaka ya Serikali inaendesha tofauti na
maono yako kwa lengo la kuleta ufanisi au ubora zaidi katika mradi husika.
“Kimsingi unaleta sasa kusudio la kuwekeza katika hilo eneo
ambalo wewe umeona kwamba mamlaka fulani ya Serikali inavyoendesha jambo fulani,
mimi ningeweza kuendesha vizuri zaidi kwa faida yangu kibiashara, kwa faida ya
Serikali kwa maana ya kutoa huduma. Hivyo sasa unaleta kusudio la kuwekeza
kwenye kituo cha Ubia, ukishaleta kituo kinaita Mamlaka ya Serikali pamoja na
wewe na kisha unawasilisha dhana yako hiyo ambayo unataka kuileta kwenye eneo
husika. Basi mchakato kutokea pale ukiwekwa sawa sawa na kuonekana inafaa unapata
fursa ya kuwekeza kwa utaratibu huo wa ubia ambao umetokana na wewe kuanzisha
fursa,” aliongeza Kamishna Kafulila.
Hivyo alibainisha kuwa Sekta Binafsi inaweza kuangalia maeneo mbalimbali, ambayo inaweza kuwekeza kwa ubia ana Serikali ikiwemo Sekta za elimu, maji, miundombinu ya barabara, afya na maeneo kadha wa kadha ambayo Sekta binafsi inaona kuna fursa ya kibiashara kama ikisimamia na kuleta faida kibiashara kwa msalhi yake yenyewe pamoja na Serikali.
Kafulila alibainisha njia ya tatu kuwa ni ile ambayo Mamlaka ya Serikali inahitaji huduma kwa haraka, ufumbuzi wa jambo fulani kwa haraka huku taratibu za kibajeti na za kimanunuzi zitachukua muda mrefu, hivyo mamlaka ya Serikali inaweza kuzungumza moja kwa moja na mwekezaji mwenye uwezo na wakaingia mkataba kutekeleza mradi husika.
“Kwahiyo Mamlaka ya Serikali inaleta tu taarifa kwa Kituo cha
Ubia, kwa mfano inasema tuna shida labda ya majosho ya kuogeshea ng’ombe na
tunaona bajeti inachelewa kutekeleza jambo hili na tunahitaji pengine ndani ya
miezi michache ijayo tuwe tunakamilisha hili jambo na mahitaji haya ni ya
haraka. Kwahiyo hii ni sifa ya mradi ambao unaweza kukafanywa kwa mazungumzo ya
moja kwa moja kwa sababu kuna muwekezaji ambaye anauwezo wa kufanya kazi hii,”
alifafanua Kafulila na kueleza,
“Huo ni mfano tu, lakini kila eneo ambalo mamlaka ya Serikali
ina uhitaji wa huduma fulani kwa haraka inaweza mamlaka hiyo kuomba kufanya
majadiliano na mwekezaji mwenye uwezo moja kwa moja bila utaratibu huu ambao
unatumika kwa maana ya ule utaratibu wa upembuzi,”.
Alisema njia ya nne ni ile ambayo inaitwa ‘special
arrangement’, kwa maana ya makubaliano maalumu au utaratibu maalumu ambao unafayika
kama kuna aina fulani ya uwekezaji ambao Serikali inauhitaji huku kukiwa na
kampuni binafsi yenye uwezo wa kuufanya, lakini utekelezaji wake unakwamishwa na
taratibu za kisheria.
“Kwahiyo aina hiyo ya uwekezaji ina ruhusu kampuni binafsi na
Mamlaka ya Serikali kutengeneza makubaliano nje ya sheria inayosimamia ubia. Hata
hivyo utaratibu huo hufanikiwa baada ya Tume ya Mipango kuridhia kwamba mradi huo
ni wa kimakakati na una mazingira maalumu, lakini pia ni lazima Mwanasheria Mkuu
wa Serikali ajiridhishe na zaidi Baraza la Mawaziri liridhie,” alieleza
Kamishna Kafulila.
Hata hivyo Kafulila alisema kuwa utaratibu huo hufanyika
kwa miradi mikubwa na yenye unyeti wake kiasi cha kukubaliana kufumua baadhi ya
vifungu vya kisheria ili kuuruhusu mradi kutekelezwa.
Kafulila alieleza kuwa mfumo huu wa ubia ni kwa faida
ya pande tatu, faida kwa mwekezaji kwa maana ya kwamba anapata biashara, faida
kwa Serikali kwa maana ya kwamba inafanikisha upatikanaji wa mradi bila kutumia
kodi, kukopa, kwahiyo inaipa fursa Serikali kufanikisha mradi husika bila presha
ya kodi na mkopo, lakini pia ni faida kwa umma kwani huduma inapatikana kwa
wakati bila kusubiri utaratibu wa Serikali kukopa na kutumia kodi.
Aliongeza kuwa, zaidi mradi wa ubia unaendeshwa na kampuni
binafsi ambayo inatengeneza faida na kulipa kodi.
No comments