Breaking News

DC Kilakala awaita watu kutembelea utalii wa majimoto Morogoro



MKUU wa Wilaya ya Morogoro  Mussa Kilakala amehamasisha jamii kujenga utamaduni wa kufanya utalii wa ndani na kutembelea vivutio vilivyopo ikiwemo kivutio cha utalii cha maji moto kilichopo katika kata ya Kisaki, kijiji cha Kisakimaji moto Wilayani Morogoro. 

Kilakala ametoa rai hiyo mara baada ya kutembelea kijijini hapo na kujionea kivutio cha chemichemi inayotoa maji ya moto muda wote bila kikomo wala kupoa kwa maji hayo hata ikinyesha mvua.

"Mwenyezi Mungu ametubariki katika maeneo yetu, tunayo chemichemi ya maji moto, muda na wakati wote iwe kipindi cha jua au mvua maji yanakuwa ya moto, hususani majira ya asubuhi maji haya yanatoka mvuke kabisa karibu wilayani kwetu katika Kijiji hiki mjionee maajabu haya makubwa" amehimiza DC Kilakala. 

"Chemichemi hii ipo Kijiji cha KisakiMajimoto, Kata ya Kisaki, Halmashauri ya Morogoro Vijijini niwakaribishe tu wananchi na Watanzania wote kutembelea Kivutio hiki cha Utalii ndani ya Wilaya yetu ya Morogoro, "alisisitiza Kilakala. 
Naye Afisa  Mali Asili Wilaya ya Morogoro Wahida Beleko amesema chemichemi za maji moto zipo pia katika baadhi ya hifadhi nchini lakini yanatofautiana ikilinganishwa kiwango cha joto kilichopo.

"Chemichemi hizi zipo maeneo mengi, yapo hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere, hata Ziwa Manyara yapo lakini ya kwetu kidogo ni tofauti, haya joto lake ni kali sana hasa majira ya asubuhi,

"Cha ajabu hata mvua ikinyesha tunatarajia kuwa yatapozwa kutokana na maji ya baridi, lakini ndiyo yanakuwa yamoto zaidi, na maji haya kitaalamu yanatibu magonjwa ya ngozi" amesema.





No comments