Breaking News

MHE. KYOBYA AWAPONGEZA WANANCHI WA IFAKARA KWA KURUDISHA MIKOPO KWA WAKATI

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Dustan Kyobya, akimuelekeza jambo Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyofanyinyika katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo uliopo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara. Pembeni kwa Bw. Kibakaya ni Afisa Sheria Mwandamizi kutoka Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Ramadhani Myonga.
Na. Ramadhan Kissimba, WF, Morogoro
 
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Dustan Kyobya amewapongeza wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Wilayani Kilombero kwa kuwa na nidhamu na mikopo waliyochukua na kuirejesha kwa wakati.
 
Mhe. Kyobya amesema hayo wakati akifungua program maalum ya Elimu ya Fedha kwa Umma inayoendeshwa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na washirika mbalimbali wa sekta ya fedha nchini iliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Maendeleo – Ifakara, Mkoani Morogoro.
 
‘’Wakina Mama mpo vizuri sana katika kurejesha mikopo mnayochukua na ndio maana uchumi wa wanawake katika mji wa Ifakara unakua kwa kasi ikilinganishwa na vijana ambao wamekuwa na tabia ya kutorejesha mikopo yao kwa wakati’’ alisema Mhe. Kyobya.
 
Aidha, aliongeza kuwa ili kupata maendeleo ya haraka ni vyema watu wakope kupitia Taasisi zilizoidhinishwa na Wizara ya Fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania, kwa kufanya hivyo wataepuka changamoto mbalimbali zinazotokana na wakopeshaji wasio rasmi ambao wamekuwa wakiwaingiza wananchi kwenye hatari ya kutaifishwa mali zao.
 
Mhe. Mkuu wa Wilaya aliwataka wananchi wa Halamshauri ya Mji wa Ifakara kuitumia vizuri fursa ya elimu ya fedha waliyoipata ili iwasaidie kutatua changamoto wanazokutana nazo kupitia mikopo hasa ile inayotolewa kwa masharti magumu na mikataba isiyoeleweka inayoandaliwa na baadhi ya watoa huduma wa fedha nchini.
 
‘’Najua kuwa mnachangomoto kubwa mnayoipata kupitia watoa huduma za fedha wasio waaminifu kwa kuwapa mikataba iliyoandaliwa kwa lugha ya kiingereza, wakati wengi wenu hamfahamu lugha hiyo, na kuna mtoa huduma za fedha mmoja nilishamfukuza Wilayani kwangu kwa kusumbua wananchi na mikopo yake isiyoeleweka’’ aliongeza Mhe. Kyobya.
 
Vilevile Mhe. Kyobya aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kuamua kutoa elimu ya fedha hasa kwa wananchi wa vijijini, na kuongeza kuwa kutokana na fursa nyingi za kilimo zilizopo Kilombero, elimu hiyo itawanufaisha wananchi wa Wilaya hiyo katika kuongeza uzalishaji wa mazo ya kilimo na kukuza Uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
 
Mhe. Kyobya aliwaagiza Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Kilosa kuhakikisha wanaratibu mafunzo ya aina hiyo yanafanyika mara kwa mara katika kata zote Wilayani Kilombero ii kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa Wilaya hiyo kuhusu mikopo umiza.
 
Program maalum ya elimu ya fedha kwa maeneo ya Mkoa wa Morogoro inalenga kuwahimiza wananchi kujiwekea akiba katika Taasisi rasmi za fedha kama vile benki nk, ili kuweza kuwa na fedha kwa ajili ya shughuli za kilimo badala ya kutumia fedha zote na Kwenda kukopa mikopo umiza wakati wa kilimo.
 
 
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha kutoka katika kata na tarafa mbalimbali za Halmashauri ya Mji wa Ifakara wakifuatilia mada zilizotolewa na watalaamu wa masuala ya fedha katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo.

No comments