Breaking News

HADIJA AKAMATWA AKIWA NA MTOTO MCHANGA ALIYEMUIBA...'MWENYEWE ADAI KUKOSA MTOTO KWENYE NDOA MBILI"



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga SACP Janeth Magomi akizungumza na waandishi wa habari - Picha Malunde
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga SACP Janeth Magomi akizungumza na waandishi wa habari

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limefanikiwa kumkamata mwanamke aliyejulikana kwa jina la Hadija Juma (24) mkazi wa Kijiji cha Sengerema wilaya ya Uyui Mkoa wa Tabora kwa tuhuma ya kuiba mtoto mchanga mwenye jinsi ya kike katika kituo cha afya Mbika Halmashauri ya Ushetu  Mkoa wa Shinyanga.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Jumamosi Agosti 24,2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga SACP Janeth Magomi amesema mtoto huyo aliibiwa Agosti 20,2024 saa 12 jioni ndipo jeshi la polisi lilianza kufanya ufuatiliaji na kufanikiwa kumkamata mwanamke huyo Agosti 22,2024 akiwa na mtoto huyo.

“Mtoto huyo alizaliwa Agosti 17,2024 katika kituo cha afya Mbika na mama yake mzazi kuendelea kuwepo katika kituo hicho kwa uangalizi baada ya kujifungua kwa njia ya upasuaji… na siku ya tukio Agosti 20,2024 majira ya saa 12 jioni wakati mama akiendelea kufanya mazoezi ndipo akabaini mtoto hayupo. Baada ya kupokea taarifa hizo ufuatiliaji wa haraka ulifanyika na Agosti 22,2024 saa tatu usiku askari walifanikiwa kumkamata Hadija Juma akiwa na mtoto huyo”,ameeleza Kamanda Magomi.

“Mtuhumiwa amehojiwa na kukiri kutenda kosa. Amesema amekuwana changamoto ya uzazi ambapo aliolewa Ushetu kwa muda wa miaka miwili hakufanikiwa kupata mtoto na ameolewa tena kwa mara ya pili Uyui Tabora hajafanikiwa kupata mtoto na kutokana na tamaa ya kupata mtoto ndiyo maana ameiba mtoto huyo. Taratibu za kumfikisha mahakamani zinakamilishwa”,ameongeza Kamanda Magomi.

 Aidha amewashauri akina mama ambao hawajabahatika kupata watoto kutokana na changamoto za uzazi waende kwa wataalamu wa afya ili kutatua changamoto hizo.  

Kamanda Magomi amewashukuru na kuwahimiza wananchi kuendelea kutoa taarifa za wahalifu na uhalifu.



from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/iyekUnQ

No comments