WASANII WA BONGO MOVIE WAJIFUNZA KWA KINA KUHUSU SEKTA YA MADINI
Baadhi ya Wasanii wa filamu maarufu Bongo Movie wamepata fursa ya kujifunza kwa kina kuhusu sekta ya madini kupitia Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Wasanii hao, Sultan Mdima, Mwajuma Ramadhani, na Seif Mbembe wameonyesha shauku kubwa katika kuelewa mnyororo mzima wa shughuli za uchimbaji madini, mchango wa sekta ya madini kwenye uchumi wa nchi sambamba na namna wanavyoweza kutumia maarifa hayo katika kazi zao za sanaa.
Aidha, wamepata maelezo ya kina kutoka kwa Wataalam wa Wizara ya Madini na Taasisi zake kuhusu mchakato ya uchimbaji, usafishaji, na kuongezea thamani madini mbalimbali kama vile Dhahabu, Almasi, Tanzanite na madini muhimu na mkakati.
Sultan Mdima, mmoja wa wasanii waliohudhuria, amesema, “Ni muhimu sana kwetu kama wasanii kuelewa sekta mbalimbali za uchumi wa nchi yetu. Hii itatusaidia kuandaa kazi za sanaa ambazo sio tu zinaburudisha bali pia zinatoa elimu kwa jamii.”
Kwa upande wake, Mwajuma Ramadhani ameongeza, “Elimu hii imenifungua macho kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya madini. Ninashukuru kwa fursa hii na ninaamini itaongeza thamani katika kazi zetu za sanaa.”
Naye, Seif Mbembe ameeleza kuwa, “Nimejifunza mambo mengi mapya ambayo naweza kusema tunaweza kuyatumia siku zijazo katika kutengeneza filamu na vipindi vya televisheni vinavyohusu maisha ya wachimbaji na sekta ya madini kwa ujumla, hii ni sekta muhimu sana”
Sanaa ya uigizaji na filamu ni daraja kati ya elimu na burudani katika sekta mbalimbali ikiwemo ya madini kwani zinaweza kuonesha hatua kwa hatua mchakato ya uchimbaji madini, kutoka kwa utafiti wa awali, uchimbaji, usafishaji, hadi usindikaji wa madini. Hii inaweza kusaidia watazamaji kuelewa jinsi madini yanavyopatikana na kuandaliwa kwa matumizi.
Pia, filamu zinaweza kuonesha jinsi sekta ya madini inavyosaidia jamii na kuchangia uchumi wa maeneo yanayohusika kwa kujumuisha fursa za ajira, maendeleo ya miundombinu, na changamoto za kiuchumi zinazoletwa na madini. Sambamba na kuangazia masuala ya haki za binadamu katika sekta ya madini, kama vile utumikishwaji wa watoto,
Vilevile, filamu zinaweza kuonesha maendeleo ya kiteknolojia katika uchimbaji wa madini, kama vile matumizi ya mashine za kisasa, roboti, na teknolojia za usalama pamoja na kueleza jinsi madini yanavyosafirishwa na kuuzwa katika soko la kimataifa, na jinsi bei za madini zinavyoathiriwa na mambo ya kiuchumi na kisiasa duniani.
Kwa njia hizo, filamu zinaweza kutoa elimu muhimu kuhusu sekta ya madini, na kusaidia watu kuelewa na kushiriki katika mnyororo wa sekta ya madini.
No comments