Breaking News

VIJIJI VYOTE NYASA VYAFIKIWA NA UMEME,Waziri Kapinga amesema TANESCO na REA zitahakikisha umeme haiishii majumbani tu bali maeneo yote ya huduma za kijamii.


Na Mwandishi Wetu 

Naibu Waziri Nishati,  Mhe. Judith Kapinga leo Julai 22, 2024 amewasha umeme katika Shule ya Sekondari Nyasa iliyopo katika Kijiji cha Chimate Kata ya Chiwanda wilayani Nyasa mkoani Ruvuma na kueleza kuwa Vijiji vyote katika Wilaya hiyo vimepelekewa huduma ya umeme.

Akizungumza na Wananchi wa kijiji cha Chimate Mhe. Kapinga amesema Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) zimejizatiti kuhakikisha kuwa huduma ya umeme haiishii majumbani tu bali  inafika kwenye maeneo yote ya huduma za kijamii. 

Ameongeza kuwa, kazi ya usambazaji umeme vijijini ilianza kwa kupeleka umeme ngazi ya vijiji na hivi sasa kazi zinaendelea kwenye vitongoji. 

"Nimefika hapa leo kwa ajili ya ajenda ya umeme, ndugu zangu maendeleo mnayoyaona yanafanyika hapa yanaendelea kufanyika nchi nzima kwani dhamira ya Serikali ni kupeleka umeme kwenye maeneo yote nchini." Amesisitiza Mhe. Kapinga

Ameongeza kuwa, Serikali imejipanga vyema  katika kutekeleza miradi ya upelekaji wa umeme kwenye Vitongoji  na kutanabaisha kuwa  maendeleo ni hatua hivyo vitongoji vyote vitafikiwa na huduma ya umeme.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Miradi ya Umeme Vijijini (REA) Mkoa wa Ruvuma, Robert Dulle amesema Wilaya ya Nyasa inajumla ya Vijiji 84 ambapo Vijiji vyote vimepata umeme kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Akiongelea upelekaji wa umeme kwenye vitongoji Mhandisi Dulle amesema kati ya Vitongoji 421, vitongoji 122 vimepata huduma ya umeme na kazi inaendelea kupeleka umeme vitongoji vilivyobaki.

Aidha, amesema kwa sasa REA inatekeleza miradi mitatu katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Nyasa.

Ametaja miradi hiyo kuwa  ni REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa pili, upelekeji wa umeme katika Viwanda, Migodi na maeneo ya kilimo na Mradi wa Ujazilizi Nzunguko wa Pili c.

No comments